Barr: Hakuna ushahidi wa madai ya wizi wa kura Marekani
2 Desemba 2020Akiyazungumzia madai yanayotolewa na timu ya kampeni na kisheria ya Rais Trump, Barr amesema hadi sasa hawajapata ushahidi wowote kuhusu udanganyifu katika kiwango ambacho kinaweza kuyaathiri matokeo yaliyompa ushindi Joe Biden. Matamshi hayo yanaonekana kama pigo kubwa kwa Trump, ambaye hajakubali kushindwa.
Barr amesema kwamba kumekuwa na madai kuhusu udanganyifu wa kimfumo na kwamba mashine zilipangwa mahsusi kwa ajili ya kuchakachua matokeo ya urais. Amesema wizara ya mambo ya ndani na wizara ya sheria zimeyachunguza madai hayo, lakini hazijapata ushahidi wowote unaoweza kuyathibitisha.
Kwa muda mrefu Barr amekuwa akionekana kuwa mtiifu kwa Rais Trump tangu alipochukua nafasi ya Jeff Sessions mwaka 2018, lakini kabla ya uchaguzi vyombo vya habari viliripoti kuhusu Trump kutoridhishwa na mwenendo wake kwamba hakuonesha juhudi katika harakati za kiongozi huyo kuchaguliwa tena kuiongoza Marekani.
Barr aliamuru uchunguzi ufanyike
Mwezi uliopita, Barr aliwaamuru waendesha mashtaka wa shirikisho kuchunguza madai yoyote ya kuaminika ya udanganyifu, kabla matokeo ya uchaguzi wa urais wa 2020 hayajathibitishwa na kuwataka wajiepushe na madai yasiokuwa ya kweli.
Muda mfupi baada ya kauli hiyo ya Barr, Trump aliandika katika ukurasa wake wa Twitter kwamba uchunguzi huo ni wa uwongo.
Soma zaidi: Trump adai kuna "wizi mkubwa" wakati hesabu zikiendelea
Wanasheria wa timu ya kampeni ya Trump, Rudy Giuliani na Jenna Ellis wameapa kuendelea kuyapinga matokeo hayo mahakamani. Giuliani amesema kwa heshima ya mwanasheria mkuu, maoni hayo yanaonekana hayana ufahamu wowote kuhusu kasoro zilizojitokeza na udanganyifu wa kimfumo uliofanyika.
''Kama mnavyojua, tangu mwanzoni kabisa, kura zilizopigwa kwa njia ya posta zilikuwa chanzo cha kutiliwa shaka kwa kiwango fulani, kama sio wasiwasi mkubwa kuhusu mazoea ya udanganyifu," alisema Giuliani.
Wakati huo huo, kiongozi wa wabunge wa chama cha Democratic katika Baraza la Seneti, Chuck Schumer amesema anahisi Barr ndiye anafuata kufukuzwa kazi na Trump, kwa sababu kiongozi huyo anaonekana kumtimua yeyote anayepingana na madai hayo.
Biden anaendelea kuipanga serikali yake
Kwa upande wake, Biden kutoka chama cha Democratic ameendelea kujikita katika kuipanga serikali yake kabla hajachukua rasmi madaraka Januari 20. Jana amelitaka bunge kuidhinisha mfuko wa kupambana na virusi vya corona ambao umekwama kwa miezi kadhaa. Aidha, ameahidi kuchukua hatua zaidi kuusaidia uchumi wa Marekani baada ya kuapishwa.
Biden kutoka chama cha Democratic kwa sasa anaongoza kwa kura 306 dhidi ya 232 zinazohitajika kushinda za Kamati ya Wajumbe Maalum, maarufu Electoral College na kulingana na idadi ya kura rasmi, Biden amemshinda Trump kwa takriban kura milioni 6.2.
Timu ya kampeni ya Trump inafanya kila liwezekanalo kupitia vyombo vya habari, mahakama na majimbo kuzuia kuthibitishwa kwa Biden Desemba 14.
Wakati huo huo, Trump ametania kwamba atagombea tena urais mwaka 2024. Akizungumza katika sherehe za sikukuu ya Krismasi zilizofanyika katika Ikulu ya Marekani na kuhudhuriwa na wajumbe wa kamati ya taifa ya chama cha Republican, Trump amesema imekuwa miaka minne mizuri katika uongozi wake.
(DPA, AP, AFP, Reuters)