1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Usalama-UN kupigia kura mswada wa Sahara Magharibi

27 Aprili 2018

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kupiga kura kuhusu mswada tete utakaozishinikiza Morocco na Polisario kurudi katika meza ya mazungumzo chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa

https://p.dw.com/p/2wntm
UN-Sicherheitsrat in New York | Abstimmung Syrien
Picha: Reuters/E. Munoz

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa leo linatarajiwa kupiga kura kuhusu mswada tete wa azimio ulioandaliwa na Marekani ambao utaweka msingi wa mazungumzo ya kusuluhisha mzozo wa Sahara Magharibi uliodumu kwa miongo mingi.

Marekani imewasilisha mswada wa azimio ambao utazishinikiza Morocco na chama cha Polisario kinachoungwa mkono na Algeria, kurudi katika meza ya mazungumzo chini ya usimamizi wa Umoja wa Mataifa.

Mswada huo uliowasilishwa wiki iliyopita utafufua jukumu la ujumbe mdogo wa Umoja wa Mataifa kuhusu usimamishaji mapigano katika Sahara Magharibi na pia kuelezea hatua za kurejea kwenye mazungumzo.

Morocco na Polisario zilipigania udhibiti wa Sahara Magharibi kuanzia 1975 hadi 1991 pale mkataba wa usitishaji mapigano ulipoafikiwa na ujumbe wa na kikosi cha Umoja wa Mataifa uliojulikana kama MINURSO ulipopelekwa kuangalia utekelezaji wa makubaliano hayo.

Baada ya Urusi na Ethiopia kulalamika kuwa yaliomo katika mswada huo yaliipendelea Morocco na hivyo ulikosa usawa, Marekani iliwasilisha marekebisho siku ya Alhamisi. Mswada huo sasa utaurefusha muda wa MINURSO kwa miezi sita badala ya mwaka mmoja. Hiyo ina maana kuwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa litaujadili tena mwezi wa Oktoba.

Chama cha Polisario kinaungwa mkono na Algeria
Chama cha Polisario kinaungwa mkono na AlgeriaPicha: DW/Nour Elhayet El Kebir

Wito kwa pande zote mbili kujitolea upya

Wanadiplomasia wamesema wanatarajia baadhi ya nchi kujizuia kupiga kura, lakini wana matumaini kuwa utapitishwa wakati wa kura.

Mswada huo wa azimio unasisitiza umuhimu wa pande zote mbili kujitolea upya kuendeleza mchakato wa kisiasa na kujiandaa na duru ya tano ya mazungumzo huku ukitilia mkazo haja ya kutambua hali halisi  pamoja na moyo wa kuridhiana.

Duru ya nne ya mazungumzo ya kutafuta suluhisho kwa mzozo wa Sahara Magharibi chini ya Umoja wa Mataifa, ilifanyika mwaka 2008.

Morocco inashikilia kuwa mazungumzo yanapaswa kulenga pendekezo la kuipa Sahara Magharibi utawala wa ndani na inapinga pendekezo la Polisario la kutaka ifanyike kura ya maoni kuhusu suala la uhuru.

Mswada huo wa azimio pia unafufua wito wa kukitaka chama cha Polisario kuondoka katika eneo la Guerguerat, ambalo inalitumia kama kinga, lililoko kusini magharibi karibu na mpaka na Mauritania, na pia kijizuie kuhamishia ofisi zake eneo la Bir Lahlou lililoko kaskazini magharibi.

Sehemu ya ujumbe wa MINURSO unaoangalia utekelezaji wa mkataba wa kusitisha vita Sahara Magharibi
Sehemu ya ujumbe wa MINURSO unaoangalia utekelezaji wa mkataba wa kusitisha vita Sahara MagharibiPicha: Getty Images/AFP/A. Senna

Mswada huo wa azimio haukuweka ratiba ya kuanza mazungumzo, lakini unatoa wito kwa pande zote mbili zirudi katika mazungumzo, kwa lengo la  kupata suluhisho la haki na la kudumu na litakalokubaliwa katika Sahara magharibi.

Risala kwa Algeria

Katika risala kwa Algeria, ambayo imekataa kujihusisha katika mazungumzo ya moja kwa moja na Morocco kuhusu Sahara Magharibi, mswaada huo unazitaka nchi jirani zijihusishe zaidi na mchakato wa mazungumzo. Algeria inahisi kushiriki kwake kutaitenga Polisario na kuugeuza mgogoro huo kuwa wa kikanda.

Mswada huo wa azimio utamuomba Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres ajiingize kati na kuzungumza na pande zote husika kama hatua ya kutuliza  mivutano na wasiwasi kuhusiana na utekelezaji wa mkataba wa usitishaji mapigano.

Mnamo mwaka uliopita, Guterres alimteua rais wa zamani wa Ujerumani na mkurugenzi mkuu wa zamani wa shirika la fedha duniani (IMF) Horst Koehler, kuwa mjumbe wake mpya kuhusu mzozo wa Sahara Magharibi  akiwa na jukumu la  kuanzisha mazungumzo mapya.

Mwanadiplomasia mmoja amesema Koehler anatarajiwa kufanya ziara mpya ya kanda hivi karibuni

Mwandishi: John Juma/AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman