Baraza la Usalama kupitisha azimio kuhusu janga la corona
26 Aprili 2020Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linatarajia kupitisha azimio hilo licha ya mivutano kati ya Marekani, China na Urusi. Jukumu hilo litatekelezwa? Jee mwito wa ushirikiano umefunikizwa na sera za kizalendo au hiyo ni hatua ya kuelekea kwenye kuubadalisha Umoja wa Mataifa ulioundwa mnamo mwaka 1945 kwa lengo muhsusi la kuzuia na kutatua migogoro ya kimataifa?
Wanadiplomasia na wataalamu waliojibu maswali ya shirika la habari la AFP hawakuonyesha matumaini makubwa. Baraza la Usalama limekuwa kimya juu ya janga kubwa kabisa lisilokuwa na kifani tangu kumalizika vita vikuu vya pili. Baraza hilo limekutana mara moja tangu kulipuka janga la corona. Lilifanya mkutano wake tarehe 9 mwezi huu wa April kutokana na pendekezo la Ujerumani na Estonia.
Lengo la Azimio:
Azimio lililopendekezwa kwa pamoja na Tunisia na Ufaransa linatoa mwito wa kuimarisha juhudi za pamoja baina ya mataifa yote pia linatoa mwito wa kukomesha uhamasa na mapigano kwenye maeneo ya mizozo. Lengo la azimio hilo ni kuunga mkono juhudi za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na mashirika kadhaa ya Umoja wa Mataifa yanayopambana ili kuzuia maakumbizi ya virusi vya corona na athari zake za kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Mkurugenzi wa kitengo cha Umoja wa Mataifa kinachoshughulikia migogoro ya kimataifa, Richard Gowan amesema baraza la uslama linajaribu kujitoa kimasomaso kwa azimio hilo ili kujionyesha kuwa limechukua hatua. Hata hivyo amesema hatua hiyo haitaleta manufaa thabiti. Jee azimio hilo litaziwajibisha nchi zote wanachama na kuleta manufaa kwenye sehemu za mizozo kama vile Syria, Yemen, Mashariki ya Kati, Afghanistan, Colombia na katika baadhi ya nchi za barani Afrika? Kukomesha miogoro duniani ni jambo linalostahili pongezi lakini changamoto iliyopo ni namna ya kufikia kwenye lengo hilo kwa kila nchi. Hayo amesema mwanadiplomasia mmoja ambae hakutaka kutajwa jina.
Wakati huo huo wanadiplomasia kadhaa wamesema azimio la baraza la usalama ni hatua muhimu sana na wamesisitiza kuwa litapitishwa na baraza hilo. Hata hivyo kizingiti kikubwa katika kuleta umoja kinaweza kusababishwa na jinsi azimio hilo litakavyolizingatia shirika la afya duniani, WHO ambalo limelaaniwa mara kwa mara na rais wa Marekani Donald Trump. Rais huyo amelalamika namna shirika hilo lilivyolikabili janga la corona. Trump amesema asasi hiyo haikuweka mambo wazi na ameamua kusimamisha mchango wa fedha wa Marekani kwa asasi hiyo, lakini China imejibu kwa kuongeza mchango wake wa fedha kwa WHO.
Mwito wa Urusi:
Mapema mwezi huu Urusi ilitoa mwito wa kuachana na sera za kuweka vizingiti, kukomesha vita vya biashara na pia imetaka kuondolewa kwa vikwazo vinavyowekwa bila ya mashauriano. Hata hivyo duru za kidiplomasia zinasena maswala hayo magumu yanaweza kusuluhishwa na wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama na hata kwa kuwashirikisha viongozi wa nchi.
Jee wanachama hao wa kudumu hawatatumia fursa iliyopo sasa kujenga mfumo mpya wa dunia baada ya janga la corona na ikiwezekana kufungua njia mpya itakayofuatwa na Umoja wa Mataifa? Mjumbe mmoja amesema juhudi hiyo inapaswa kuongozwa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.
Binadamu bilioni saba na nusu duniani wanahitaji sera ya pamoja katika wakati huu wa sasa kuliko wakati mwingine wowote. Profesa kwenye chuo cha mitaala ya siasa mjini Paris Bertrand Badie amesisitiza hayo. Hata hivyo ametanabahisha juu ya sera za kutetea maslahi ya kitaifa ambazo amesema zimeongezeka duniani.
Chanzo:/AFP