Baraza la Ulaya Laitimua Urusi
16 Machi 2022Uamuzi huo unakuja baada ya wiki kadhaa za kulaani vitendo vya Urusi nchini Ukraine. Wakati hayo yakiendelea Rais Zelensky wa Ukraine ametoa wito wa Urusi kufikishwa mahakama ya kimataifa kwa kile alichokiita vitendo vya kigaidi katika ardhi ya Ukraine.
Katika taarifa ya kamati ya mawaziri kutoka mataifa 47 yanayounda baraza hiloimesema kuwa imethibitisha Urusi kufukuzwa uanachama kuanzia leo baada ya miaka 26 ya uanachama, uamuzi huo unakuja baada ya wiki za kulaani vitendo vya Urusi huko Ukraine.
Soma Pia:Msimamo wa NATO unaweza kubadilika Urusi ikitumia silaha za nyuklia?
Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergey Lavrov mapema leo katika mahojiano ya televisheni amesema kuwa kulikuwa hakuna budi kuondoshwa kwenye chombo hicho na kuishutumu NATO na nchi za Ulaya kwa kutumia vibaya wingi wao katika chombo hicho ambacho Ukraine pia ni mwanachama.
Katika mtandao wake wa Twitter waziri wa mambo ya nje wa Ukraine Dmytro Kuleba ameipongeza hatua hiyo.
Urusi:Yaendeleza msururu wa mashambulizi
Urusi imeendelea kufanya mashambulizi yake katika miji muhimu, huku mamia ya raia wakiendelea kulikimbia taifa hilo. Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy ametoa wito wa Urusi kufikishwa katika mahakama ya kimataifa kwa kile alichokiita vitendo vya kigaidi katika ardhi ya Ukraine.
Zelenskyy ametoa wito kwa viongozi wa dunia kuitambua Urusi kama serikali ya kigaidi akisisitiza kwamba kwa kutofanya hivyo "haitawezekana kurejesha haki kwa Ukraine na utaratibu wa dunia." Alisema katika video yake
Soma Pia:Watu wanne wauawa katika mashambulizi ya leo Kiev
Aliongeza Urusi imegeuka kuwa gaidi wa kweli asiekuwa na aibu lakini itawajibika kwa kila kitu kinachotokea hivi sasa Ukraine, ambapo hali mbaya ya kiutu imekuwa ikishuhudiwa katika miji ambayo Urusi imekuwa ikishambulia kimkakati, ikiwemo mji wa bandari wa Mariupol.
"Ulimwengu unaanza kutambua Urusi ni serikali ya kigaidi haitawezekana kurejesha haki kwa Ukraine."Alisema Zelensky.
Kwa mujibu wa Ukraine hadi kufikia leo Jumatano vikosi vya Urusi vimendelea kushambulia miji ya Ukraine na miundombinu, na kuharibu vituo 400 vya elimu na kuua watoto 103.
Duru za ndani ya Ukraine zinaarifu kuwa Mwendesha mashtaka mkuu wa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai, Karim Khan, ametembelea Ukraine leo jumatano na kufanya mikutano ya mtandaoni na Rais wa Ukrain Volodymyr Zelenskiy.
Zelensky: Ahutubia Bunge la Marekani
Katika hotuba yake iliogubikwa na huzuni nyingi kwa bunge la Marekani (Congress) Zelensky ambae mara zote amekuwa katika mstari wa mbele akipigania taifa lake ameliomba taifa hilo msaada zaidi wakati taifa lake likiendelea kushuhudia hali mbaya ya kiutu wakati huu Urusi inapoendeleza mashambulizi katika maeneo muhimu.
Amesema vita hivyo havilihusu tu taifa lake, bali pia vinahusiana na thamani ya Ulaya na ulimwengu wote. Huku akiendelea kulisisitiza bunge hilo kulitazama upya ombi lake la kufungwa kwa anga la taifa lake ama Marekani kupeleka ndege za kivita lisaidia taifa lake kutokana na Urusi kulibadilisha anga la Ukraine na kuwa chanzo cha vifo vya maelfu ya watu.
Katika hotuba yake alioitoa kwa njia ya video amemwambia Rais Joe Biden wa Marekani kwamba kama kiongozi wa taifa kubwa ulimwenguni angelitamani kuona anawaangaluia wa Ukraine katika kipindi hiki kigumu wanachopitia
Soma Pia:Marekani, washirika wazidisha shinikizo la kiuchumi kwa Urusi
Rais Joe Biden wa Marekani baadae hii leo anatarajiwa kutangaza msaada wa dola milioni 800 kwa Ukraine baada ya rais Zelensky kuomba msaada wa kijeshi kukabiliana na uvamizi wa Urusi wakati akilihutubia bunge la Congress.
Ufadhili huo mpya utatoa msaada wa ziada wa kibinadamu na usalama kwa Ukraine taifa ambalo bado linakabilia na hali mbaya zaidi ya kiutu kutokana na mashambulizi ya Urusi.