1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la Seneti Marekani lauridhia mkataba na Urusi

23 Desemba 2010

Baraza la seneti la Marekani liumeridhia mkataba mpya wa kupunguza umiliki wa vichwa vya nyuklia kati ya nchi hiyo na Urusi uitwao START

https://p.dw.com/p/zofx
Seneta John Kerry alisimama kidete kuhakikisha baraza linaukubali mkataba wa START ,Picha: AP

Maseneta 71 walipiga kura kuukubali huku 26 wakiukataa, ukiwa ni ushindi wa theluthi mbili ya kura zote.

Mkataba huo mpya utazifanya Urusi na Marekani kukubaliana kupunguza idadi ya vichwa vya kinyuklia kote duniani, ambapo kila nchi itakuwa na vichwa kiasi ya 1500.

Marais Barack Obama na Dmitry Medvedev wa Urusi walitia saini makubaliano ya mkataba huo April mwaka huu ya kupuguza idadi ya vichwa hivyo vya kinyuklia katika kipindi cha miaka saba ijayo kwa takriban 30 asilimia.

Mkataba wa mwanzo uliotiwa saini mwaka 1991 muda wake ulimalizika Disemba mwaka jana.

Rais Obama aliupongeza mshikamano uliooneshwa na maseneta wa chama cha upinzani cha Republik ambao baadhi yao walipiga kura kuunga mkono mkataba huo, na kusema ni hatua kubwa katika kuhakikisha usalama wa dunia.

Obama Pressekonferenz Ratifizierung Start Abrüstungsabkommen NO FLASH
Rais Barack ObamaPicha: AP

´´Haya ni makubaliano ya maana kuwahi kufikiwa katika kudhibiti silaha, kwa takriban miongo miwili na yatatufanya tuwe salama na kupunguza vichwa vyetu vya nyuklia pamoja na Urusi´´ aliongeza Rais Obama, na kusisitiza

´´Katika mkataba huu wakaguzi wetu pia watarejea katika kambi za kinyuklia za Urusi, kwa hivyo tutakuwa katika nafasi ya kuamini, lakini pia kuthibitisha.Tutaendelea kuimarisha uhusiano wetu na Urusi, uhusiano ambao ni muhimu katika changamoto zilizoko za kuweka vikwazo vikali zaidi dhidi ya Iran, ili kuzuia silaha za nyuklia zisiangukie katika mikono ya magaidi´´

Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov mbali ya kuipongeza hatua hiyo ya baraza la seneti la Marekani, amesema, nchi yake inahitaji muda kuudurusu kabla ya bunge lao, Duma, kuuridhia.

Bundeskanzlerin Angela Merkel besucht Afghanistan
Kansela Angela MerkelPicha: dapd

Viongozi kadhaa duniani wameipongeza hatua hiyo, ambapo Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Waziri wa Mambo ya Nje Guido Westerwelle wameelezea matumaini yao kuwa Urusi itauridhia mkataba huo haraka iwezekanavyo.

Nchini Japan serikali ya nchi hiyo na ile ya mji wa Hiroshima pia wameipongeza hatua hiyo.Mji wa Hiroshima mwaka 1945 ulishambuliwa na Marekani kwa bomu la kwanza la Atomik, ambapo inakadiriwa watu 140,000 walikufa papo hapo.

Mjini New York, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amesema anaamini hatua hiyo ya Marekani itasaidia kasi iliyofikiwa katika miaka ya hivi karibuni ya upunguzwaji wa silaha za nyuklia.

Mwandishi:Aboubakary Liongo/DPA/AFP/ZPR

Mhariri:Thelma Mwadzaya