1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baraza la mawaziri la Burundi lakutana kikao cha dharura

Saleh Mwanamilongo
11 Juni 2020

Kikao cha dharura cha baraza la mawaziri la Burundi kinafanyika mjini Bujumbura, ili kujadili mustakbali wa taifa hilo siku tatu baada ya kifo cha ghafla cha Rais Pierre Nkurunziza kinachoonekana kuacha ombwe la uongozi.

https://p.dw.com/p/3ddEC
Burundi Stadtansicht Bujumbura
Picha: Imago/Xinhua Afrika

Kikao hicho kitaongozwa na naibu rais wa Burundi, Gaston Sindimwo. Duru kutoka serikali ililiambia shirika la habari la AFP kwamba kikao hicho kitajadili mchakato wa uongozi wa taifa kufuatia kifo cha ghafla cha Pierre Nkurunziza. Na serikali kuifahamisha rasmi korti ya katiba kuhusu pengo lililoachwa kwenye wadhifa wa urais.

Nkurunziza aliefariki Jumatatu akiwa na umri wa miaka 55,alikuwa anajiandaa kumkabidhi madaraka rais mteule kutoka chama chake cha CNDD/FDD aliechaguliwa mwezi uliopita.Lakini kifo chake kimezuwa hofu kuhusu hatma ya kisiasa ya nchi hiyo ambayo ilishuhudia machafuko ya vita vya wenyewe kwa wenyewe,vilivyo sababisha wimbi la wakimbizi.

Katiba inasemaje?

Gaston Sindimwo, Vizepräsident von Burundi
Makamu wa kwanza wa rais wa Burundi Gaston SindimwoPicha: DW/A. Niragira

Kwa mujibu wa katiba ya Burundi, spika wa bunge,Pascal Nyabenda ndiye anatakiwa kuapishwa kuongoza nchi kwa kipindi cha mpito hadi atakapo apishwa rais mteule mwezi Agosti.

Hatua itakayo fuatwa itachukuliwa sio na mawaziri bali na kamati ya dharura ambayo inajumuisha baadhi ya majenerali wa jeshi wenye ushawishi mkubwa,ilielezea duru hiyo ya serikali.

Moja wa viongozi wa chama tawala cha CNDD/FDD, ameliambia shirika la AFP kwamba serikali inatarajia kuharakisha sherehe za kuapishwakwa rais mteule badala ya kuwepo na kipindi cha mpito.Licha ya kazi kuendelea kufanyika,serikali ilitangaza msiba wa kitaifa wa siku saba ambapo bendera zinapepea nusu mlingoti.

Pascal Nyabenda, CNDD-FDD-Partei Burundi
Pascal Nyabenda spika wa bunge la BurundiPicha: C. de Souza/AFP/GettyImages

Nkurunziza aliiongoza Burundi kwa kipindi cha miaka 15 na aliamini sana maswala ya kidini,na mwenyewe kujiita mchungaji.

Baadhi ya maafisa wa chama chake wanaelezea kifo cha Nkurunziza kama janga kwa nchi hiyo.Lakini hakuongoza taifa hilo peke yakee,na wadadisi wanahisi kwamba huenda kukazuka vita vya madaraka ndani ya chama chake.

Taarifa za kuaminika zinaelezea kwamba Nkurunziza alipendelea spika wa sasa wa bunge kumrithi lakini majenerali wa jeshi walimuunga mkono jenerali Evariste Ndayishimiye.

Mke wa Nkurunziza, Denise Bucumi, ambae alikuwa akitibiwa ugonjwa wa Corona jijini Nairobi, Kenya alirejea jumanne mjini Bujumbura.