1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baerbock aanza ziara ya siku mbili Finland, Sweden

13 Februari 2023

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Ujerumani Annalena Baerbock anaanza ziara ya siku mbili katika nchi jirani za Ulaya Kaskazini Finland na Sweden. Itajikita katika uwanachama wa NATO na upelekaji wa silaha Ukraine

https://p.dw.com/p/4NQUc
Belgien | EU-Außenministertreffen
Picha: Virginia Mayo/dpa/AP/picture alliance

Ziara hiyo itajikita zaidi kwenye jitihada zilizokwama za nchi hizo mbili jirani za Kaskazini mwa Ulaya kujiunga na Jumuiya ya Kujihami ya NATO na pia suala la kupelekwa silaha nchini Ukraine. 

Akiwa katika mji mkuu wa Finland Helsinki, Baerbock amepangiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Kigeni Pekka Haavisto, pamoja na kuruzu mojawapo ya vituo vya ulinzi wa raia vilivyojengwa chini ya ardhi.

Hapo kesho, ziara ya Baerbock itaendelea hadi mji mkuu wa Sweden Stockholm.

Baada ya miongo mingi ya kutoegemea upande wowote, Finland na Sweden zilituma maombi ya kujiunga na muungano wa ulinzi wa kijeshi wa nchi za Magharibi kama jibu kwa uvamizi wa Urusi ncnhini Ukraine karibu mwaka mmoja uliopita.

NATO unterzeichnet Beitrittsprotokolle für Finnland und Schweden
Finland na Sweden zinasubiri idhini ya kujiunga na NATOPicha: Kenzo Tribouillard/AFP

Lakini ili nchi ijiunga na NATO, panahitajika idhini ya nchi zote 30 wanachama. Uturuki na Hungary bado hazijaidhinisha maombi hayo.

Idhini ya Hungary inatarajiwa kutolewa lakini Uturuki imeibua pingamizi kadhaa, ikiwemo kuituhumu Sweden kwa kutochukua msimamo imara dhidi ya Wakurdi na makundi mengine yanayozingatiwa kuwa ya kigaidi.

Mazungumzo ya Baerbock huenda pia yakaangazia uwasilishwaji unaopangwa nchini Ukraine wa vifaru vya kivita vya Leopard 2 vilivyotengenezwa Ujerumani, ambavyo Sweden na Finland zinamiliki.

Serikali ya Ujerumani inatafuta kukuza kundi la washirika wenye nia ya kupeleka vifaru Kyiv.

Waziri Mkuu wa Finland Sanna Marin aliiambia redio moja nchini humo kuwa serikali yake haijafanya uamuzi kuhusu suala hilo alilolielezea kuwa gumu. Alisema Finland ina mpaka mrefu wa kilomita 1,300 na Urusi – ukweli ambao lazima uzingatiwe wakati wa kufanywa maamuzi ya kusafirisha silaha.

Sweden pia haijaamua kuhusu upelekaji wa vifaru nchini Ukraine. Waziri Mkuu Ulf Kristersson pia hajafuta uwezekano wa nchi yake kupeleka Ukraine ndege za kivita wakati fulani katika siku za usoni, lakini anasema suali hilo sio la dharura kwa Sweden ikizingatiwa kuna nchi hiyo ina suala muhimu la kujiunga na NATO.

Wakati huo huo, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Jens Stoltenberg amesema anatarajia suala la ndege za kivita kujadiliwa katika mkutano wa siku mbili wa mawaziri wa Ulinzi wa NATO kuanzia kesho.

Stoltenberg pia amesisitiza kuwa nchi za NATO zinazopeleka ndege za kivita nchini Ukraine hazitaifanya NATO kuwa sehemu ya mzozo huo

DPA