Azimio la Lugano la kuijenga upya Ukraine latiwa saini
5 Julai 2022Wakihitimisha mkutano wa siku mbili katika jiji la kusini mwa Uswizi la Lugano, viongozi kutoka nchi zaidi ya 40 na mashirika ya kimataifa kama vile benki ya uwekezaji ya Ulaya na shirika la ushirikiano wa kiuchumi na maendeleo (OECD) wametia saini azimio la Lugano linaloweka kanuni za kuijenga upya Ukraine.
Ahadi zimekaribishwa kwa furaha
Wawakilishi kwenye mkutano huo pia wamekaribisha ahadi za kutoa misaada ya kisiasa, kifedha na kiufundi na wakati huo huo wamezindua kanuni za Lugano zitakazoongoza juhudi za ujenzi, ambao Ukraine inasema unaweza kugharimu hadi dola bilioni 750.
Kanuni hizo zinajumuisha ushirikiano kati ya Ukraine na washirika wake wa kimataifa na zinazingatia mageuzi ya ndani. Nchi nyingi zimeazimia kuiunga mkono Ukraine kupitia kile kinachotarajiwa kuwa ni ahueni ya muda mrefu na ya gharama kubwa, na zimekubaliana juu ya mahitaji ya mageuzi mapana ili kuongeza uwazi na vita dhidi ya ufisadi.
Umoja wa Ulaya umesema Ukraine bado inahitaji kufanya maendeleo katika maeneo kama utawala wa sheria, kuwadhibiti matajiri wachache kwenye utawala, kuondoa upendeleo katika kutoa zabuni kwenye miradi ya ujenzi, kupambana na rushwa na kuhakikisha haki za msingi.
Miongoni mwa nchi zilizotia saini
Miongoni mwa nchi zilizotia saini azimio hilo ni pamoja na Marekani, Uingereza, Ufaransa na Japan na wakati huohuo nchi hizo zimelaani uvamizi wa kijeshi wa Urusi dhidi ya Ukraine na ziitaka Moscow iondoe wanajeshi wake kutoka kwenye ardhi ya Ukraine mara moja.
Rais wa Uswisi Iganzio Cassis, aliyeandaa mkutano huo pamoja na Ukraine, katika hafla ya kuufunga mkutano huo amepongeza azimio lililofikiwa na amesema ni hatua muhimu ya kwanza katika njia ndefu ya kuirejesha Ukraine kwenye hali yake ya kawaida.
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema uharibifu wa nyumba, shule, hospitali, na miundombinu mingine muhimu itachukua miaka kadhaa kujengwa upya.
Guterres ameongeza kusema kuwa wajibu wa Umoja wa Mataifa ni kuiunga mkono serikali ya Ukraine katika shughuli za kuokoa maisha, kuimarisha juhudi za kutoa misaada, kuendeleza mpango wa uokoaji na maendeleo wa Ukraine, na kulinda mafanikio yaliyopatikana kuelekea malengo ya maendeleo endelevu.
Azimio hilo la Lugano linajikita katika kujitolea kwenye mchakato wa kidemokrasia utakaohusisha sehemu zote za kijamii. Malengo yakiwa ni pamoja na kuibadilisha Ukraine kuwa mahala pa jamii iliyo kwenye mazingira safi yasiyo na hewa ukaa, na kuifanya nchi hiyo kuwa ya kidijitali.
Vyanzo: AFP/RTRE/DPA