1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azimio la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa leo latimiza miaka 60

Mohamed Dahman10 Desemba 2008

Malengo yake yote hayakutimizwa lakini Azimio la Haki za Binaadamu Duniani limeendelea kubakia muhimu zaidi leo hii kuliko wakati lilipopitishwa miaka 60 iliopita.

https://p.dw.com/p/GCnQ
Waziri Mkkuu wa zamani wa Pakistan marehemu Benazir Bhutto miongoni mwa watunukiwa wa Tuzo ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa.Picha: AP

Umoja wa Mataifa leo hii unaadhimisha miaka 60 tokea kuanza kutumika kwa azimio hilo hapo tarehe 10 mwezi wa Desemba mwaka 1948 mjini Paris Ufaransa na kuwakilisha makubaliano ya kwanza kabambe miongoni mwa mataifa yenye kufafanuwa hususan haki na uhuru wa binaadamu.

Umoja wa Mataifa unaliona azimio hilo lina mustakbali mzuri.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Mkuu wa masuala ya haki za binaadamu mjini Geneva imesema katika taarifa kwamba misingi ya azimio hilo la haki za binaadamu imejitokeza katika katiba na sheria za zaidi ya nchi 90.

Hata hivyo imesema kwa watu wengi azimio hilo la dunia limeendelea kubakia kuwa ahadi isiotimizwa kutokana na nia za kisiasa za serikali kutimiza wajibu wao kuburuza miguu katika kutekeleza ahadi hizo.

Hali hiyo hivi karibuni imezidi kuwa mbaya kutokana na mgogoro wa fedha unaoendelea kuiathiri dunia ambao umewatumbukiza mamilioni ya watu duniani kwenye umaskini.Haki ya mtu kujipatia chakula na uzima wa afya ni muhimu sawa na uhuru wa kujieleza na kuabudu.

Katika mkesha wa kuamkia siku ya leo ya miaka 60 ya Azimio la Haki za Binaadamu Duniani Shirika la Umoja wa Mataifa la Kilimo cha Chakula FAO limeripoti kwamba idadi ya watu wanaokabiliwa na njaa imeongezeka na kufikia milioni 963 ikiwa zaidi kwa milioni 40 kuliko ilivyokuwa mwaka jana kutokana na kupanda kwa bei za vyakula.

Taarifa ya ofisi ya haki za binaadamu ya Umoja wa Mataifa inasema hakuna nchi duniani inayoweza kubweteka na kusema wamefiika walipokusudia katika kutimizwa kwa malengo ya azimio hilo.Imesema mamilioni ya watu duniani kote hata hawajuwi kwamba wana haki wanazoweza kuzidai kutoka serikali zao ambazo ni sehemu kuu za azimiho hilo lililoandaliwa na washiriki wa Marekani wakiongozwa na mke wa rais wa wakati huo nchini Marekani Eleanor Roosevelt baada ya vita vikuu vya pili vya dunia.

Umoja wa Mataifa ukiungwa mkono na makundi ya utetezi umekuwa na mikutano iliodumu kwa mwaka mzima kuzipa nguvu upya juhudi za kutekeleza azimio hilo. Utekelezaji wa haki za binaadamu umekuwa ukihesabiwa kama njia mjarabu kabisa ya kuzuwiya maangamizi mengine kama yale ya Wayahudi yaliofanywa na manazi wa Ujerumani na kuweka utaratibu wa kimataifa kuwalinda maskini, wafanyakazi wahamiaji na wakimbizi.

Haki za binaadamu sambamba na maendeleo na usalama ni nguzo tatu ambazo kwayo Umoja wa Mataifa imekuwa ikiendesha harakati zake tokea kuundwa kwake hapo mwaka 1945.

Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa la nchi wanachama 192 litawatunuku Tuzo ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binaadamu kwa mwaka 2008 watu sita wawili wakiwa marehemu.Miongoni mwa watunukiwa hao ni kamishna wa zamani wa haki za binaadamu wa Umoja wa Mataifa Louise Abhor,waziri mkuu wa zamani wa Pakistan marehemu Benazir Bhutto aliyeuwawa wakati akiwa katika kampeni ya uchaguzi hapo mwaka 2007 na mtawa marehemu Dorothy Stang wa Ufaransa.

Leo hii Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa litakuwa na mikutano kujadili mafunzo waliojifunza katika miongo iliopita, changamoto za hivi sasa na mpango wa kusonga mbele.

Umoja wa Mataifa umeutangaza mwaka 2009 kuwa mwaka wa kimataifa Kujifunza Haki za Binaadamu katika juhudi za kunufaika na shinikizo la utekelezaji mkubwa zaidi wa azimio la haki za binaadamu duniani.