Azimio la Baraza la Usalama dhidi ya Makaazi ya Wayahudi
27 Desemba 2016Tunaanza lakini na azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya ujenzi wa makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi katika ardhi za wapalastina-azimio lililoungwa mkono na wanachama 14 wa baraza la Usalama huku Marekani kwa mara ya kwanza kabisa ikiamua kutotumia haki yake ya kura ya turufu na badala yake kujizuwia kupiga kura . Maoni ya wahariri wa magazeti ya Ujerumani yanatofautiana kuhusu azimio hilo. Gazeti la "Badische Neueste Nachrichten" linaandika: "Ushindi wa kihistoria wapalastina waliousherehekea baada ya azimio la baraza la usalama, hauna maana yoyote. Kwanza kwasababu azimio hilo lililopitishwa na wanachama 14, huku Marekani ikijizuwia kupiga kura, kisheria si lazma lifuatwe. Pili, Israel inaweza kutegemea mageuzi katika siasa ya Marekani kuelekea Mashariki ya kati, Barack Obama atakapomaliza mhula wake mwezi january mwakani. Atakaeshika nafasi yake, rais mteule Donald Trump ameshasema kupitia mtandao wa kijamii Twitter,"msimamo wa serikali yake utakuwa mwengine " atakapoingia madarakani january 20 mwakani.
Siasa mpya ya marekani kuelekea Mashariki ya kati
Mhariri wa gazeti la "Die Rheinpfalz" analiangalia kwa jicho jengine kabisa azimio la baraza la usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi katika maeneo ya wapalastina. Gazeti linaandika: "Haikuwa dhidi ya Israel pale Barack Obama alipoamua kutotumia kura ya turufu kuzuwia azimio la baraza la usalama la Umoja wa mataifa dhidi ya Israel, linaloutaja mpango wa Israel wa kujenga makaazi ya wahamiaji wa kiyahudi katika ardhi za wapalastina kuwa kinyume na sheria na pingamizi kwa amani. Rais wa Marekani anakubaliana na maoni ya mataifa yote ya dunia na kumfichua waziri mkuu wa Israel kuwa ni mwongo. Alijinata siku chache zilizopita kwamba uhusiano wa kimataifa kwa dola hilo la kiyahudi...haujawahi kunawiri kama unavyonawiri hivi sasa. Kwamba marais wa zamani wa Marekani mara kadhaa waliachia maazimio dhidi ya Israel yapite, serikali ya Netanyahu inaonyesha imesahau.
Hatua kali zaidi za ulinzi
Zaidi ya wiki moja baada ya shambulio la kigaidi la mjini Berlin, sauti zinazidi kupazwa kudai hatua za ukaguzi zizidishwe makali. Gazeti la "Schwarzwälder Bote" linaandika: "Mjadala wa kisiasa umehanikiza kufuatia shambulio la mjini Berlin ambapo kila mmoja anashauri hatua bora zaidi za kinga dhidi ya ugaidi. Kuanzia ukaguzi kupitia video hadi kufikia kurejeshwa mwakao watuhumiwa. Ila ni machache tu yanayotajwa kuhusu udhaifu uliojitokeza katika kadhia ya Anis Amri. Masuala kadhaa hayajapatiwa majibu ....Hatua za aina gani maafisa wa usalama wanahitaji ili kuweza kuwadhibiti wale wanaotajwa kuwa "watuhumiwa hatari? "Na kwanini zoezi la kuwarejesha makwao watu waliokataliwa kinga ya ukimbizi humu nchini kila mara linadhihirika kua mfano wa chui asiyekuwa na meno?
Mwandishi: Hamidou Oumilkheir/Inlandspresse
Mhariri: Mohammed Khelef