1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azerbaijan yamkamata rais wa zamani wa Nagorno-Karabakh

5 Oktoba 2023

Azerbaijan imethibitisha hivi leo kwamba imemkamata rais wa zamani wa serikali iliyojitangazia uhuru wa jimbo la Nagorno-Karabakh, ambayo kwa sasa imekubali kujivunja na kuwa sehemu ya Azerbaijan.

https://p.dw.com/p/4X9Bx
Ruben Vardanyan -ehemaliger Separatistenführer aus Berg-Karabach von aserbaidschanischen Sicherheitsbeamten festgenommen
Picha: State Border Service of Azerbaijan/Handout/AFP

Tamko la serikali ya Azerbaijan lilifuatia taarifa iliyotolewa siku ya Jumatano (Oktoba 4) na serikali ya Armenia ambayo ililaani vikali Baku kwa kuwashikilia mamia ya viongozi waliokuwa wanawania kujitenga kwa jimbo la Nagorno-Karabakh.

Ofisi za mwendesha mashitaka na usalama wa taifa za Azerbaijan zilisema siku ya Alkhamis (Oktoba 3) kwenye tamko lao la pamoja kwamba Arayik Harutyunyan alitiwa nguvuni siku ya Jumanne kwa "tuhuma za kuanzisha vita dhidi ya Azerbaijan na uhalifu wa kivita."

Soma: Scholz azungumza na rais wa Azerbaijan kujadili mzozo wa Nagorno-Karabakh

Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 49 alikuwa ndiye rais wa serikali ya jimbo hilo wakati wa mapigano ya mwaka 2020 kati ya Azerbaijan na Armenia kuwania udhibiti wa Karabakh, na alijiuzulu mwezi uliopita, siku chache kabla ya Baku kuanzisha operesheni yake ya kijeshi. 

Wawakilishi wengine kadhaa wa serikali ya zamani ya Karabakh pamoja na makamanda wa kijeshi wametiwa nguvuni na Baku, akiwemo Ruben Vardanyan, bilionea aliyeoiongoza serikali ya jimbo hilo baina ya Novemba 22 na Februari mwaka huu.

Armenia yajitosa kuwatetea

Wizara ya mambo ya nje ya Armenia imesema itachukuwa hatua zozote iwezazo kulinda haki za wawakilishi wa Nagorno-Karabakh ambao wameshikiliwa na Baku, ikiwemo kwenda kwenye mahakama za kimataifa.

Armenien Yerevan | Premierminister Nikol Pashinyan
Waziri Mkuu wa Armenia, Nikol Pashinyan.Picha: Tigran Mehrabyan/AP/picture alliance

Viongozi wa serikali iliyotaka kujitenga na Azerbaijan walikubali kuweka silaha chini, kuivunja serikali yao na kuwa sehemu ya Azerbaijan kufuatia operesheni kali ya siku moja ya Baku mwishoni mwa mwezi uliopita.

Soma: Kiongozi wa Azerbaijan kutohudhuria mazungumzo kuhusu Karabakh huko Uhispania

Ingawa serikali kuu mjini Baku inaendelea na mazungumzo ya kuwaingiza viongozi wa Karabakh na wapiganaji wao kwenye serikali rasmi, lakini Mwendesha Mashitaka Mkuu Kamran Aliyev amesema kuwa uchunguzi wa makosa ya uhalifu umeanzishwa dhidi ya maafisa 300 wa serikali ya zamani ya Karabakh.

Ofisi ya Haki za Binaadamu ya Umoja wa Mataifa imeitaka Baku kuwapatia wafungwa hao haki zao zote na ulinzi kamili. 

Aliyev, Erdogan wagomea mkutano wa Ulaya

Wakati huo huo, Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan na mwenzake wa Uturuki, Tayyip Erdogan, walikwepa kuhudhuria mkutano kilele wa viongozi wa Ulaya unaofanyika mjini Granada nchini Uhispania kuanzia Alkhamis. 

Ilham Aliyev - Nikol Pashinyan - Charles Michel
Kutoka kushoto: Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan, Rais Charles Michel wa Baraza la Ulaya na Waziri Mkuu Nikol Pashinyan wa Armenia.Picha: Dursun Aydemir/AA/picture alliance

Ofisi ya rais wa Azerbaijan ilisema kiongozi wao amegoma kuhudhuria mkutano huo kutokana na upendeleo wa wazi wa baadhi ya wajumbe wa mkutano huo, akiitaja Ufaransa ambayo imesema iko tayari kuisaidia Armenia hata kijeshi. 

Soma zaidi: Bunge la Armenia laidhinisha nchi hiyo kujiunga na ICC

Kukosekana kwa Rais Aliyev kunavunja matumaini ya viongozi wa Umoja wa Ulaya kutumia jukwaa hilo ili kuendeleza juhudi za kidiplomasia kuzipatanisha tena Azerbaijan na Armenia, baada ya Baku kulitwaa rasmi jimbo la Nagorno-Karabakh.

Hii ni mara ya pili kwa Rais Erdogan, ambaye ana nafasi kubwa kwenye mzozo wa Armenia na Azerbaijan, kuacha kuhudhuria mkutano kama huu.

Vyanzo: AP, dpa, AFP