1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Australia na jumuiya ya ASEAN zaweka makubaliano mapya

27 Oktoba 2021

Makubaliano hayo yataimarisha zaidi mahusiano ya diplomasia na usalama baina ya pande hizo mbili.

https://p.dw.com/p/42FuB
ASEAN Summit 2021 I Scott Morrison I Australien
Picha: Lukas Coch/AAP/imago images

Australia na nchi wanachama wa jumuiya ya kusini mashariki mwa Asia (ASEAN) zimekubaliana kuanzisha mkakati kabambe wa ushirikiano, hiyo ikiwa ni ishara ya azma ya Canberra kuwa na ushawishi au mchango mkubwa katika kanda hiyo.

Makubaliano hayo yataimarisha zaidi mahusiano ya diplomasia na usalama baina ya pande hizo mbili.

Japo maelezo mahsusi ya makubaliano ya Australia na ASEAN hayakutangazwa moja kwa moja, Waziri Mkuu wa Australia Scott Morrison ameahidi kwamba nchi yake itayaunga mkono.

"Kama mjuavyo Australia, Uingereza na Marekani hivi karibuni zilitangaza makubaliano ya ushirikiano yajulikanayo kama AUKUS. Nchi zote tatu ni washirika wa ASEAN kwa mashauriano. Na ninataka kuzungumzia hilo kwa sababu uwazi na mawasiliano kuhusu hili ni muhimu kwa Australia na marafiki wetu wa ASEAN," amesema Morrison. 

Mwanzo mpya wa mahusiano?

Brunei ambayo ndiyo mwenyeji wa mkutano huo imesema makubaliano hayo yanaashiria mwanzo mpya wa mahusiano na yatakuwa yenye maana na tija kwa pande zote.

​​
​​Picha: Adam Schultz/White House/ZUMA Wire/imago images

Australia imesema itawekeza dola milioni 154 kufadhili miradi ya afya, nishati, usalama, kupambana na ugaidi na uhalifu na kutoa nafasi za masomo kwa mamia ya wanafunzi katika kanda hiyo.

Eneo la kusini mashariki mwa Asia limekuwa kanda ya makabiliano ya kimkakati kuhusu ushindani wa Marekani na China.

Marekani na washirika wake wamekuwa wakizidisha ushikaji doria kukabili idadi kubwa ya manowari na vyombo vingine vya kivita vya China baharini. Beijing hupeleka vyombo hivyo kama njia ya kutilia mkazo madai yake ya kumiliki sehemu kubwa ya bahari ya kusini mwa China.

China pia inataka kushirikishwa kwa kiwango sawa kwenye mpango huo wa kimkakati. Waziri Mkuu Li Keqiang alikutana na viongozi wa ASEAN na rais wake Xi Jinping anatarajiwa kukutana na viongozi wa jumuiya hiyo katika mkutano maalum wa kilele mwezi Novemba. Duru za kidiplomasia zimeliarifu shirika la habari la Reuters.

Baadhi ya meli za kivita za Marekani katika pwani ya Taiwan.
Baadhi ya meli za kivita za Marekani katika pwani ya Taiwan.Picha: U.S. Coast Guard/AP/picture alliance

Fumio Kishida aelezea wasiwasi kuhusu China kujitanua kijeshi

Kwenye mkutano huo, Waziri Mkuu wa Japan Fumio Kishida amewasisitizia viongozi wa nchi za kusini mashariki mwa bara Asia kwamba nchi yake inapinga vikali changamoto dhidi ya biashara huru na sheria kuhusu mipaka huru ya baharini, huku akielezea wasiwasi wa kanda hiyo juu ya kuimarika kwa nguvu za kijeshi za China.

Kishida amesema pia kwamba amegusia masuala kuhusu hali za haki za binadamu Hong Kong na Xinjiang, pamoja na umuhimu wa amani na utulivu wa Taiwan

Taharuki imekuwa ikiongezeka Taiwan ambako China inadai ni milki yake inayopaswa kuchukuliwa hata kwa nguvu ikibidi. Lakini Taiwan inasema ni taifa huru na itatetea uhuru wake na demokrasia yake.

Rais wa Marekani Joe Biden na Waziri Mkuu wa China Li Keqiang leo wamehudhuria mkutano wa kilele wa nchi za kusini mashariki mwa bara Asia ASEAN kwa njia ya video.

Fumio Kishida, Waziri Mkuu wa Japan.
Fumio Kishida, Waziri Mkuu wa Japan.Picha: Handout/AFP

Vyanzo vya mivutano ASEAN

Miongoni mwa masuala ambayo yamekuwa yakisababisha mvutano katika kanda hiyo ni pamoja na ongezeko la ushindani kati ya Marekani na China kuhusu biashara, demokrasia, Taiwan, na visa vya kichochezi vya China katika maeneo yanayozozaniwa. 

Kishida alihudhuria mkutano huo kwa njia ya video ambao awali ulijadili pia hofu zinazotokana na shughuli za kijeshi na makabiliano katika bahari ya kusini mwa China. Alitoa wito wa kukamilishwa kwa utaratibu wa mahusiano kati ya ASEAN na China kuambatana na sheria ya kimataifa.

Mnamo mwaka 2016, mahakama ya kimataifa ya usuluhishi wa migogoro, ilibatilisha madai ya China yaliyopishana na Malaysia, Vietnam, Taiwan, Ufilipino na Brunei.

Makubaliano yaliyoafikiwa mwezi uliopita kati ya Uingereza, Marekani na Australia kuhusu Australia kumiliki nyambizi zinazotumia nishati ya nyuklia, yamezidisha hofu ya nchi za kusini mashariki mwa Asia kujilimbikizia silaha.

Awali mkataba wa AUKUS kati ya Marekani, Uingereza na Australia ulisababisha mzozo na Ufaransa.
Awali mkataba wa AUKUS kati ya Marekani, Uingereza na Australia ulisababisha mzozo na Ufaransa.Picha: Andrew Harnik/abaca/picture alliance

Joko Wodido ana mashaka na mkataba wa AUKUS

Rais wa Indonesia Joko Widodo amesema alikuwa na wasiwasi mkataba huo ujulikanao kama AUKUS unaweza kuchochea uhasama katika kanda hiyo, kulingana na waziri wake wa mambo ya nchi za nje Retno Marsudi.

Ufilipino inauunga mkono mkataba wa AUKUS lakini rais wake Ridrigo Duterte alisema siku ya Jumatano kwamba, lazima mkataba huo uwe na tija wala si kuvuruga ushirikiano uliopo.

Australia tayari ina mikataba ya kimkakati kuhusu masula mbalimbali na Indonesia, Malaysia, Thailand, Singapore, Ufilipino na Vietnam.

Viongozi wengine wanaohudhuria mkutano huo ni pamoja wakuu wa India, Australia, New Zealand, Urusi, Korea Kusini, Marekani na China.

(RTRE, APE)