Assad ajigamba kupambana Syria
12 Septemba 2016Huku muda mchache tu ukiwa umebakia kabla ya kuanza kwa mpango wa kusitisha mapigano uliofikiwa na Marekani na Urusi, Bashar Al Assad ameapa kuyarejesha maeneo yote yaliyotekwa na waasi na kuiweka Syria chini utawala mmoja.
Akijigamba rais Bashar Al Assad alionekana katika televisheni ya taifa pale alipoutembelea mji wa Daraya ambao kwa muda mrefu ulikuwa umetekwa na waasi, katika mahojiano pembeni ya barabara Assad alisema ana mkakati wa kurejesha kila eneo la Syria kutoka mikononi mwa magaidi
Ukimya juu ya kusitisha mapigano
Wakati wote katika mahojiano hayo Bashar Al Assad hakutaja chochote kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano.
Makubaliano hayo yanatarajiwa kuanza muda mfupi ujao kuanzia sasa na yakifanikiwa kuwepo, mpango wa kuwafikishia watu misaada ya kibinadamu unatarajiwa kuimarika na kwa upande mwingine Marekani na Urusi zitaungana pamoja katika zoezi la kupambana na makundi ya Kiislamu yenye msimamo mkali. Juhudi hizi lakini zinakabiliwa na changamoto lukuki ikiwemo changamoto ya juu ya kutenganisha baina ya wapinzani wa kweli wanaopigania haki na demokrasia nchini Syria na waasi wanaounga mkono makundi ya kigaidi. Wapinzani wanadai kuwa mpango huo mzima wa kusitisha mapigano unaipendelea serikali ya Assad ambayo hadi kufikia sasa inaonekana kuwa yenye uwezo zaidi kuliko wao ukilinganisha na wakati mapigano yalipoanza, wanasema nguvu za upande wa serikali zimedi kutokana na msaada wa kijeshi wa Urusi na Iran.
Hatua za kuweka chini silaha
Makubaliano ya hivi sasa ni ya pili yaliyofikiwa na Marekani na Urusi katika mwaka huu ya kwanza yalikuwa mwezi Februari mwaka huu ambayo hayakudumu huku pande zote mbili zikirushiana lawama za kukiuka makubalaiano.
Marekani inaunga mkono baadhi ya makundi ya waasi lakini sasa inataka kubadili mtazamo wake kuhusianana na swala zima la mapigano nchini Syria hasa katika juhudi za kupambana na kundi linalojiita dola la Kiislamu IS ambalo limeyateka maeneo kadhaa nchini Syria na vile vile kundi hilo halimo katika makubaliano ya kusitisha mapigano
Marekani imesema kwamba serikali ya Syria haitofanya mashambulio katika maeneo waliyokubaliana kwa kisingizio cha kuwafuata magaidi na kuwshambulia kutoka katika kundi la Al Nusra Front ingawa waasi wanadai kuwa kuna uwezekano wa serikali ya Assad kukiuka agizo hilo na hivyo kuendelea kuwashambulia kwa kutumia ndege za kivita.
Kwa mujibu wa habari kutoka kwa naibu waziri wa mambo ya nje wa Urusi, ni kwamba serikali ya Syria na wapinzani wa huenda wakakutana mwezi Oktoba katika duru nyingine ya mazungumzo ya amani.
Mwandishi: Zainab Aziz/Reuters/DPA/
Mhariri: Yusuf Saumu
.