Askofu Tutu afariki dunia
26 Desemba 2021Rais Cyril Ramaphosa ametangaza tanzia hiyo leo akimtaja Askofu Tutu kama kiongozi aliyekuwa dira ya kimaadili ya nchi hiyo.
Ramaphosa amesema kifo hicho ni ukurasa mwingine wa majonzi kwa taifa hilo wakati likimuaga kiongozi huyo wa kizazi maalum cha ukombozi wa Afrika Kusini.
Tutu alituzwa Tuzo ya Amani ya Nobel kufuatia mapambano yake yasiyo ya vurugu dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi mnamo mwaka 1984.
Hata baada ya kuangushwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi, mpiganiaji uhuru huyo aliendelea na harakati zake akikosoa mapungufu ya tawala za Afrika Kusini na visa vya ukiukwaji wa haki za binaadamu popote duniani.
Yeye ndiye alinzisha neno maarufu la “Rainbow Nation”, yaani taifa la rangi ya upinde wa mvua, akimaanisha Afrika Kusini wakati Nelson Mandela alipokuwa rais wa kwanza mweusi nchini humo.
Viongozi ulimwenguni watuma risala za rambirambi
Viongozi mbalimbali ulimwenguni wanaendelea kutuma risala za rambirambi kufuatia kifo cha Askofu Desmond Tutu wa Afrika Kusini kilichotokea mapema leo.
Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson, amesema amesikitishwa mno na kifo cha Tutu, akimtaja kama kiongozi aliyekuwa muhimu katika kumaliza utawala wa ubaguzi wa rangi na aliyechangia mwanzo mpya wa Afrika Kusini.
Akiandika kwenye ukurasa wake wa Twitter, Johnson ameongeza kwamba Tutu atakumbukwa kwa uongozi wake wa kidini bila kusahau sifa yake ya ucheshi.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta, amemuomboleza Tutu akisema aliwatia moyo kizazi cha viongozi wa Afrika, waliokumbatia falsafa yake ya kupigania ukombozi bila ya vurugu.
Mary Robinson, ambaye ni mwenyekiti wa kundi la wazee kutoka sehemu mbalimbali ulimwenguni wanaofanya kazi ya amani na haki za binaadamu, amesema wamepata pigo kubwa kufuatia kifo cha Desmond Tutu.
Robinson, ambaye pia ni rais wa zamani wa Ireland, ameongeza kuwa, Tutu alimtia moyo kuwa kile alichokitaja kuwa ‘mfungwa wa matumaini’.
Wakfu wa Nelson Mandela, Baraza la Makanisa ulimwenguni, rais wa zamani wa Marekani Barrack Obama na kiongozi wa kanisa Katoliki Ulimwenguni Papa Francis, ni miongoni mwa wale waliotuma risala zao za rambirambi.