1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asasi za kiraia zapambana na ugaidi licha ya kushutumiwa

5 Agosti 2024

Asasi za kiraia za kusini mwa jangwa la Sahara zimeanza kushirikiana na mamlaka za kisheria na mashirika ya kifedha kupambana na ufadhili wa ugaidi, lakini zenyewe hunyanyaswa kwa kisingizio cha kufadhili ugaidi.

https://p.dw.com/p/4j8QF
Mmoja wa washiriki wa kongamano la kukabiliana na ugaidi na utakatishaji fedha kusini mwa Jangwa la Sahara lililofanyika Kampala, Uganda.
Mmoja wa washiriki wa kongamano la kukabiliana na ugaidi na utakatishaji fedha kusini mwa Jangwa la Sahara lililofanyika Kampala, Uganda.Picha: DPI/DW

Kulingana na wadau waliokuwa wanashiriki kongamano jijini Kampala, utakatishaji fedha una mahusiano makubwa na ufadhili unaowawezesha magaidi kuendesha maovu yao.

Dhana hii ilianza kupata umaarufu baada ya shambulio lililofanyika Marekani tarehe 11 mwezi Septemba mwaka 2001. Tangu wakati huo, mamlaka za usalama za mataifa na kimataifa zimezidisha juhudi za kushughulikia uhalifu wa kimataifa wa utakatisaji fedha ambapo miamala hasa kwa asasi za kiraia hufuatiliwa.

Soma zaidi: Kenya kuongoza vita dhidi ya ugaidi Afrika Mashariki

Hata hivyo, katika hatua hiyo ya kupambana na ufadhili kwa ugaidi, mamlaka zimekuwa zikizigandamiza asasi za kiraia. Pesa za baadhi ya asasi kutoka kwa wafadhili zimefungiwa katika baadhi ya nchi kwa kisingizio kwamba zinatumiwa kufadhili ugaidi.

''Wanatuweka sisi katika mazingira ya kutaka kutumika vibaya. Tumeona asasi za kiraia akaunti zao za benki zikifungwa mfano Tanzania na Uganda. Wamesumbuliwa kwa kutumia mifumo hii ambayo imekuja kwa nia nzuri, lakini wako baadhi ya watawala wanaoitumia kuzinyamazisha asasi za kiraia zinazopigania masuala ya haki za binadamu, utawala bora, rushwa na kadhalika.'' Anasema mwanasheria Onesmo Paul Olengurumwa, mratibu wa Muungano wa Watetezi wa Haki za Binadamu nchini Tanzania.

Uhasama baina ya asasi na mamlaka

Katika kongamano hilo imebainika kuwa njia muhimu ya kupambana na ufadhili kwa shughuli za kigaidi ni kuondoa uhasama kati ya mamlaka za serikali na asasi za kiraia.

Matokeo ya mashambulizi ya kigaidi kaskazini mwa Msumbiji.
Matokeo ya mashambulizi ya kigaidi kaskazini mwa Msumbiji.Picha: Roberto Paquete/DW

Aidha, mashirika ya kifedha kama vile benki yamehusishwa ili kuwa na jukwaa la pamoja la kuhakikisha kuwa haki za asasi za kiraia zinaheshimiwa kwa mujibu wa shughuli za kuhamisha fedha zao. 

Soma zaidi: Marekani kuisaidia Tanzania kiusalama

''Tukikubali kwamba ugaidi ni shida kwa binadamu, asilimia 50 ya kutatua shida hii itakuwa imeeleweka. Ndiyo maana ili asasi za kiraia zifahamu kiwango cha changamoto za kudumisha usalama, tunahitaji kuwashirikisha ili nao watueleze hofu zao zinazotuhusu.'' Alisema mkurugenzi wa Kitengo cha Kupambana na Ugaidi katika Jeshi la Polisi la Uganda, David Wasswa.

Jumuiya ya wanahabari nayo ilihusishwa katika mjadala husika kwani wakati mwingine vyombo vya habari hutuhumiwa na kulipwa na magaidi na wafadhili wao, kwa lengo la kunadi harakati zao au kuzuia taarifa zinazowahusu.

''Wanahabari wenzetu wengine wako hapa kuhakikisha kwamba kero yetu pia inasikilizwa.'' Alisema Joseph Wemakor, mratibu wa asasi inayolinda haki za wanahabari nchini Ghana.

Kongamano hilo la siku mbili liliwashirikisha pia wajumbe kutoka jumuiya za kiuchumi kama vile Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) ili kuhakikisha kuwa serikali za mataifa hayo nazo zinatilia maanani njia za kuzuia ufadhali kwa shughuli za kigaidi kupitia mipaka ya mataifa yao.