Armstrong anapojitahidi kusafisha jina
17 Januari 2013Jambo linalotarajiwa hasa katika mahojiano kati ya Armstrong na Oprah, ni endapo bingwa huyo aliyenyang'anywa mataji yake aliyoshinda kwa miaka saba, anaweza kusafisha jina lake kama mdanganyifu aliyewashambulia na kuwanyamanzisha kwa miaka kadhaa wale waliomtilia mashaka. Daniel Borochof, mwanzilishi na rais wa shirika linalofuatilia mashirika ya hisani la CharityWatch, anasema wafadhili wa taasisi ya saratani ya Livestrong, ambayo Armstrong aliianzisha, walivunjwa moyo si tu na ukweli kuwa Armstrong alikuwa anatumia dawa za kuongeza nguvu, bali pia na juhudu zake za kuwanyamazisha waliokuwa wakimtuhumu kwa kufanya hivyo.
Maadui wakubwa wa Armstrong
"Baadhi ya mashambulizi yake yalikuwa dhidi ya watu waliokuwa wanaeleza tu ukweli juu ya kile kilichokuwa kinaendelea - kama anakiri hilo sasa, basi itakuwa vigumu kwa watu kuja kukubaliana naye," alisema Borochof. Miongoni mwa wale waliolengwa kama maadui wa Armstrong alikuwa Betsy Andreu, mke wa Frankie Andreu, waliyekuwa pamoja kwenye timu. Mwanamke huyo anasema Armstrong alimuonyesha kama mtu mwenye kisasi na husda pale alipotoa ushahidi wakati wa kusikilizwa kwa kesi ya kisheria, kuwa alimskia Armstrong akiwaambia madaktari waliokuwa wanamtibu saratani yake mwaka 1996 kuwa alitumia dawa za kuongeza nguvu.
"Ningependa akiri kuwa tukio la hospitalini lilikuwa la kweli," Betsy Andreu aliiambia televisheni ya ESPN wiki hii, baada ya taarifa kuwa Armstrong amekiri kutumia dawa za kuongeza nguvu katika mahojiano yake na Oprah Winfrey siku ya Jumatatu. Mahojiano haya yanarushwa kwa awamu mbili siku ya Alhamis na Ijumaa, kupitia kituo binafsi cha Oprah, cha OWN na mtandao wake wa intaneti.
Kuanzia kwa Emma O'Reilly, mtaalamu wa matibabu aliyetoa ushahidi kwa shirika la kuzuia matumizi ya dawa za kuongeza nguvu kuhusu matumizi ya dawa hizo katika timu ya Armstrong, hadi kwa Mkurugenzi wa shirika hilo, Travis Tygart, hakuna aliyeachwa katika wale wote waliomtuhumu Armstrong. Katika kujiandaa kwa mahojiano na Winfrey, Armstrong ameomba radhi kwa wafanyakazi wa shirika lake la Livestrong, na kwa baadhi ya watu katika fani ya uendeshaji baiskeli na waandishi wa habari ambao walizozana naye katika siku zilizopita.
Baadhi wamemtaka atoe zaidi ya maneno. Kampuni ya bima ya SCA, ambayo aliishtaki waliposhikilia fedha zake za bakhshishi kiasi cha dola za Marekani milioni 5 baada ya ushindi wake wa sita mwaka 2004 kutokana na madai ya kutumia dawa za kuongeza nguvu, sasa inahitaji arudishe fedha hizo. Gazeti la Sunday Times nalo linamshtaki ili arudishe fedha alizolipwa katika kesi ya kuchafuliwa jina, baada ya gazeti hilo la Uingereza kuchapicha taarifa juu ya madai ya kutumia dawa za kuongeza nguvu.
Bingwa wa kumudu wakosoaji
Mwenazake katika timu, Floyd Landis, ambaye alimtuhumu Armstrong kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu baada ya yeye (Landis) kupoteza taji lake la Tour de France mwaka 2006 kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu, alifukuzwa kwa udanganyifu na kukosa uaminifu. Mwingine, Tyler Hamilton, aliwaambia maafisa wa serikali kuwa ana hofu baada ya kutoa ushahidi katika baraza la majaji lililoitishwa kuchunguza matumizi ya dawa za kuongeza nguvu katika fani ya uendeshaji baiskeli, ambapo mhusika mkuu alikuwa Armstrong. Wakati huo, Hamilton alikuwa amemtuhumu waziwazi Armstrong kupitia mahojiano aliyoyafanya na kituo cha Televisheni cha CBS.
Bingwa mara tatu wa mashindano ya Tour de France, Greg LeMond, mkosoaji mkubwa wa Armstrong, ambaye anakiri kuwa tatizo la matumizi ya dawa za kuongeza nguvu linakwenda mbali zaidi ya ndugu yake huyo, alisema mbinu alizotumia Armstrong zimeharibu mchezo huo. "Kuna tofauti kubwa kati ya mtu kama Ivan Basso (ambaye alisimamishwa kwa miaka miwili kwa kutumia dawa za kuongeza nguvu) na Armstrong," LeMond alisema mwaka 2010 na kuongeza kuwa" Basso hawatishii watu! Linapokuja suala la kuwamudu watu vilivyo, Armstrong ndiye bingwa asiye na mpinzani."
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/afpe
Mhariri: Joseph Nyiro Charo