Armenia na Azerbaijan kuchukua hatua za kurejesha uhusiano
8 Desemba 2023Umoja wa Ulaya umesema unapongeza hatua hiyo na kuitaja kuwa muhimu sana kuelekea kwenye amani katika eneo ambalo linakabiliwa na migogoro kwa muda mrefu. Chini ya makubaliano hayo Azerbaijan imesema itawaachilia huru wanajeshi 32 wa Armenia huku Armenia ikiahidi kuwa itawaachia wanajeshi wawili wa Azerbaijan.
Nchi hizo mbili zimesema katika taarifa ya pamoja kwamba zinaamini kuwa ipo nafasi ya kihistoria ya kufikia amani iliyosubiriwa kwa muda mrefu. Nchi hizo mbili zimesema zinakusudia kurekebisha uhusiano kati yao na kufikia makubaliano ya amani katika mkataba utakaozingatia misingi ya heshima kulingana na kanuni za uhuru na uadilifu wa kikanda.
Hadi tamko hilo la leo Ijumaa, nchi hizo mbili zilikuwa zinazozana vikali kuhusu mchakato wa amani na kulikuweko na hali ya kutoaminiana.
Soma:Armenia na Azerbaijan zakubaliana msingi wa mkataba wa amani
Vilevile nchi hizo hazikukubaliana kuhusu nchi gani katika eneo la Ulaya mashariki itakayokuwa mwenyeji wa mkutano wa hali ya hewa mwaka ujao wa 2024. Lakini sasa zimefikia maelewano na katika sehemu ya makubaliano hayo, Armenia imekubali kuondoa pingamizi yake juu ya Azerbaijan kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa kimataifa wa mwaka ujao kuhusu mabadiliko hali ya hewa.
Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel amepongeza na kusifu makubaliano hayo kuwa ni ya mafanikio makubwa. Michel pia amesema ameukaribisha mpango wa kuwaachilia wafungwa na hivyo kuashiria nafasi kubwa ya mwanzo ambao haujawahi kutokea wa mazungumzo ya kisiasa kati ya pande hizo mbili. Michel ametoa wito kwa Armenia na Azerbaijan kukamilisha makubaliano ya amani haraka iwezekanavyo.
Marekani pia imeukaribisha mpango huo, ikisema kubadilishana kwa wafungwa wa kijeshi ni hatua muhimu inayojenga ujasiri wakati pande zhizo mbili zikiendelea kukamilisha hatua za kufikiwa makubaliano ya amani na kurejesha uhusiano wa kawaida kati yao.
Uturuki pia imepongeza makubaliano kati ya mahasimu wakubwa Armenia na Azerbaijan hatua ya kubadilishana wafungwa wa kivita na kufanya kazi katika kurejesha uhusiano uliovunjika miongo kadhaa kutokana na mzozo katika eneo la Nagorno-Karabakh.
Vyanzo:AP/RTRE/AFP