1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ari ya kibiashara imeimarika Ujerumani na Ufaransa

Saleh Mwanamilongo
24 Septemba 2020

Nia ya kibiashara nchini Ujerumani na Ufaransa imeimarika kwa mwezi wa tano mfululizo mnamo mwezi huu wa Septemba.

https://p.dw.com/p/3ixdN
Symbolbild Eurobonds
Picha: picture alliance/dpa/Bildagentur-online/HRI-McPhoto

Hali hiyo inaleta matumaini kwamba nchi hizo mbili zenye uchumi mkubwa kwenye mataifa yanayotumia sarafu ya Euro yamejiimarisha kiuchumi, licha ya janga la virusi vya corona, lililoathiri uchumi katika robo ya kwanza ya mwaka huu.

Takwimu zilizotolewa Alhamisi na taasisi ya kiuchumi ya Ujerumani ya Ifo ya mjini Munich, na taasisi ya takwimu za kitaifa ya Ufaransa zinaelezea kwamba nchi hizo mbili zishuhudia kukuwa kwa uchumi wake katika robo ya mwisho ya mwaka 2020, lakini matarajio hayo yanagubikwa na ongezeko la maambukizi na vizuwizi vipya katika kupambana na janga la COVID-19.

Taasisi ya Ifo ilielezea kwamba faharasa zake za biashara zinaonyesha kukuwa kwa alama 93.4 ukilinganisha na mwezi Agosti ambayo ilikuwa 92.5. Ni matokeo ya juu kabisa toka mwezi Februari ambapo alama ilikuwa ni 95.9.

Uchumi wa Ujerumani unastawi

Infogafik Wachstumsprognose EURO Zone DE

Rais wa taasisi ya Ifo, Clemens Fuest anasema kwamba uchumi wa Ujerumani unastawi licha ya ongezeko la idadi ya maambukizi ya virusi vya corona.

Uchumi wa Ujerumani ulijiimarisha kwa asilimia 9.7 kwenye robo ya pili ya mwaka 2020, wakati ambapo mauzo ya vifaa vya nyumbani, uwekezaji wa viwanda na biashara vilizorota kutokana na janga la virusi vya corona. Tangu mwezi Machi, serikali ilichukuwa hatua kadhaa katika kufufua uchumi, kupitia mikopo mikubwa ili kupunguza athari za virusi vya corona.

Nchini Ufaransa faharasa ya imani ya biashara iliongezeka hadi 92 mwezi huu ukilinganisha na alama 90 mwezi uliopita, na kufikia kiwango chake cha juu kabisa toka mwezi Februari, kabla ya taifa hilo kuweka vizuwizi vya miezi miwili kwa ajili ya kupambana na janga la virusi vya corona.

Faharasa ya sekta ya viwanda iliimarika kwa kasi hadi alama 96, kutoka 92. Kuimarika huko kwa hali ya kiuchumi nchini humo kumeonekana wakati ambapo serikali ya nchi hiyo haikuwa na namna nyingine isipokuwa kuogeza marufuku ya mikusanyiko kutokana na kuongezeka kwa visa vya virusi vya corona ambavyo vimefikia idadi ya juu.