Anis Amri hakuonekana kitisho kwa maafisa
29 Desemba 2016Inadaiwa kwamba dakika chache kabla Amri hajaligonga gari lake aliloteka nyara katika soko la Krismass mjini Berlin, alituma ujumbe wa sms , akisema : " Ndugu zangu, kila kitu kiko sawa , kwa mujibu wa mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Hivi sasa niko katika gari , niombeeni ndugu zangu, niombeeni."
Ujumbe huo , pamoja na picha ya kujipiga aliyoipiga akiwa ndani ya lori hilo, huenda ilitumwa kwa Mtunisia mwenye umri wa miaka 40 aliyekamatwa mjini Berlin jana Jumatano, limeandika gazeti la Sueddeutsche Zeitung.
Wachunguzi wanaotafuta kugundua iwapo Amri alikuwa na mshirika wamesema mtuhumiwa aliyekamatwa raia wa Tunisia "anaweza kuwa alihusika katika shambulio hilo". Lakini maafisa wa Ujerumani wamemwachia huru mtu huyo mwenye umri wa miaka 40 raia wa Tunisia leo, siku moja baada ya kukamatwa.
Maafisa wa kupambana na ugaidi wana taarifa za kina kuhusu Amri, walifahamu kuwa anahusiana kwa karibu na mtandao wa Waislamu wenye itikadi kali nchini Ujerumani na aliwahi kuwa anatafuta maelekezo katika mtandao juu ya jinsi ya kutengeneza mabomu ya mabomba, gazeti hilo limeripoti.
Maelezo ya hivi karibuni kabisa ya Amri, ambayo ni pamoja na taarifa kuhusiana na utambulisho wake unaotofautiana mara nane, ulifanyiwa mapitio Desemba 14, siku tano tu kabla ya kuuwa watu 12 katika shambulio la mjini Berlin.
Waendesha mashitaka magharibi mwa Ujerumani wamesema wamefungua uchunguzi wa udangayifu mapema mwaka huu dhidi ya Anis Amri , mtuhumiwa mkuu katika shambulio la wiki iliyopita mjini Berlin.
Waziri Mkuu wa Italia, Paolo Gentiloni amesema leo kwamba mtuhumiwa wa shambulizi dhidi ya soko la Krismasi mjini Berlin hakuwa anasaidiwa na mtandao wa washirika nchini Italia.
Gentiloni aliwaeleza waandishi habari mjini Rome kwamba hadi hivi sasa hakuna ushahidi kwamba kijana huyo mwenye umri wa miaka 24 raia wa Tunisia alikuwa na mahusiano na mtandao wowote nchini Italia ambao ulikuwa ukimsaidia.
Wakati huo huo polisi mjini Kolon imepiga marufuku maandamano ya kundi la siasa kali za mrengo wa kulia katika mkesha wa mwaka mpya wakati wakijaribu kuzuwia kurejewa kwa ghasia za mwaka jana na kusema wataweka vizuwizi kuzuwia mtu yeyote kuweza kuendesha gari kwa lengo la kuwashambulia watu.
Maafisa wa jiji tayari wamekwishatangaza mipango ya kuweka polisi 1,500 mara 10 zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka jana wakati polisi waliposhindwa kuzuwia uporaji na mashambulizi ya kingono ambayo wanalalamikiwa watu wenye asili ya kigeni.
Mwandishi: Sekione Kitojo / Ape / Afpe / Rtre
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo