1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Angola and UN Office of the High Commissioner for Human Rights

Nijimbere, Gregoire26 Mei 2008

Baraza la Umoja wa mataifa linalohusika na haki za binaadamu, limeitaka serikali ya Angola kufutilia mbali hatua yake ya kuifunga ofisi ya kamishina mkuu wa Umoja wa mataifa anayehusika na haki za binaadamu nchini Angola

https://p.dw.com/p/E6Pf
Bendera ya Angola


Baraza la Umoja wa mataifa linalohusika na haki za binaadamu, limeitaka serikali ya Angola kufutilia mbali hatua yake ya kuifunga ofisi ya kamishina mkuu wa Umoja wa mataifa anayehusika na haki za binaadamu nchini Angola kabla ya mwezi huu kumalizika.


Wakati serikali ya Angola ilipotangaza miezi miwili iliopita hatua hiyo ya kutaka kuifunga ofisi ya kamishina mkuu wa Umoja wa mataifa kuhusu haki za binaadamu nchini Angola kabla ya mwezi huu kumalizika, ilisisitiza kwamba mnamo miaka iliopita, ofisi hiyo ilikuwa ikihitajika lakini kwamba kwa sasa hivi amani na demokrasia vimeenea na taasisi za kitaifa zinazohusika na maswala ya haki za binaadamu zinafanya kazi kikamilifu.

Hali kadhalika serikali ya Angola ilisema hakuna sheria inayohalalisha ofisi hiyo ya kamishina mkuu wa Umoja wa mataifa anayeshughulikia maswala ya haki za binaadam kuweko nchini Angola, na kwamba kwa jumla hakuna utaratibu wowote kisheria unaofuatiliwa katika kuunda ofisi za aina hiyo isipokuwa tu misingi ya kisiasa.

Kulingana na mkurugenzi wa kitengo cha Afrika katika shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Rights Watch bi Georgette Gagnon, Angola imerudi nyuma kuhusu nia yake ya kuunga mkono mjadala na ushirikiano na Ofisi ya Umoja wa mataifa kama ilivyoahidi, nchi hiyo ikiwa pia mwanachama wa Baraza la Umoja wa mataifa kuhusu haki za binaadamu.

Bi Juliette De Rivero wa shirika hilo la Human Rights Watch aliyeko mjini Geneva Usuisi, amekwenda mbali zaidi kwa kuielezea wasi wasi juu ya msimamo huo wa serikali ya Angola:


Clip.............Juliette de Rivero

" Tuna wasi wasi kwa sababu hatua hiyo imekuja miezi mitatu tu kabla ya uchaguzi. Ni muhimu Angoka ikatoa mwanya kuweza kukosolewa kuhusu hali ya haki za binaadamu ikihitajika. Tunahofia kwamba kuifunga ofisi hiyo kunalenga zaidi kuwazuwia watu wengine wasiwezi kufuatilia kwa karibu na kutoa maoni yao juu ya hali halisi ya haki za binaadamu nchini humo".


Daima kwa maoni ya shirika la Human Rights Watch, amani haijapatikana bado katika jimbo linalopigania mjitengo na Angola la Cabinda na mashirika ya kitaifa kuhusu haki za binaadamu kama vile kamati za kimkoa bado kufanya kazi wakati serikali ikiendelea kuvibana vyombo vya habari kwa jumla. Ama kuhusu hoja ya serikali ya Angola kwamba ofisi hiyo ya Umoja wa mataifa juu ya haki za binaadamu nchini Angola ni haramu, Human Rights Watch limesema shughuli za Ofisi hiyo zilihahalishwa na mapatano yaliyofuatia kuondoka kwa wajumbe wa Umoja wa mataifa kulinda amani mwaka wa 2003.

Mashirika kadhaa ya kutetea haki za binaadamu yamelielezea shirika la Human Rights Watch kwamba ofisi hiyo ya Umoja wa mataifa juu ya haki za binaadamu ilikuwa na jukumu kubwa na kwamba iliyasaidia mashirika hayo kwa njia mmoja ama nyingine kuboresha mazingira ya kikazi na kukabiliana na vitisho kutoka kwa serikali.

Ndio sababu shirika la Human Rights Watch limeitaka serikali ya Angola kubatilisha hatua yake kuifunga ofisi hiyo ya Kamishina mkuu wa Umoja wa mataifa kwa ajili ya haki za binaadamu.

Hii haikuwa mara yake ya kwanza serikali ya Angola kutishia kuyafuta kazi mashirika ya kutetea haki za binaadamu kama ilivyotokea pia mwaka wa 2007. Shirika la Human Rights Watch kwa upande mwingine limeitaka serikali ya Angola kuyapa nafasi kubwa mashirika ya kiraia kuweza kufanya kazi kabla na baada ya uchaguzi wa mwezi Septemba mwaka huu.