Angola kuachana na DRC
21 Juni 2017Angola, taifa lenye nguvu kisiasa na kijeshi katika ukanda huo, kwa nyakati tofauti imekuwa ikimuunga mkono Kabila, ambaye aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya kuuawa kwa baba yake.
Lakini hivi sasa Angola imekuwa ikitatizwa namna kiongozi huyo wa DRC anavyoshughulikia migogoro kadhaa, ikiwemo kushindwa kuondoka madarakani wakati muhula wake ulipomalizika Desemba mwaka jana na mzozo ambao umesababisha wakimbizi kukimbilia nchi za jiani ikiwemo Angola.
Mwezi Desemba Angola iliondoa wakufunzi wa kijeshi iliokuwa imewatuma nchini Congo, ambako vita iliwaua mamilioni ya watu na kushirikisha nchi za jirani.
Uamuzi huo uliibua wasiwasi ikiwa Luanda itakuwa tayari kumuunga mkono tena Kabila na hofu hiyo imeongezeka baada ya mabadiliko ya msimammo katika mahusiano yake, kuashiria uwepo wa mageuzi makubwa katika siasa za ukanda huo.
Waziri wa mambo ya nje Georges Chikoti aliweka wazi mwezi Mei kuwa uvumilivu ulikuwa unafika mwisho wakati alipohoji kauli ya Congo ya kusema mgogoro katika jimbo la Kasai linalopakana na Angola kuwa umetatuliwa baada ya miezi kadhaa. Chikoti pia aliunga mkono wito wa uchunguzi wa kimataifa kuhusu mauaji ya wachunguzi wawili wa Umoja wa Mataifa katika mkoa huo, hatua ambayo Kinshasa iliikataa.
Changamoto ya moja kwa moja inatoka kwa mfanyabiashara wa Congo Sindika Dokolo ambaye amemuoa binti bilionea wa Rais Jose Eduardo dos Santos.
Tangu awali akiwa amejibainisha wazi kuhusu siasa za kitaifa, Dokolo katika wiki za hivi karibuni amekuwa akimshambulia Kabila kupitia mtandao wa Twitter na katika mahojiano, akiweka ulinganisho na utawala wa kiimra wa Mobutu Sese Seko.
Dokolo ametoa wito kwa wanafunzi na viongozi wa kanisa kumpinga Kabila huku akimsifu Moise Katumbi, kiongozi wa upinzani aliyeko uhamishoni.
Dokolo anasema anatoa maoni kama mwananchi wa kawaida wa Congo. Lakini hata hivyo maneno yake yanabeba uzito mkubwa kwasababu yanatoka kinywani mwa ndugu wa familia ya dos Santos.
Congo taifa lenye wakazi zaidi ya milioni 80, ambalo ni mzalishaji mkubwa wa chuma aina ya Kobalti duniani, shaba na almasi na mafuta, limekumbwa na vita na kukosekana kwa usalama tangu kuanguka kwa dikteta Mobutu mwaka 1997.
Angola imekuwa na tofauti zake na Congo katika kipindi cha nyuma, ikiwemo mzozo wa mpaka wa baharini na ushindani wa mafuta pamoja na kufukuzwa kwa maelfu ya Wachimba almasi wa Congo nchini Angola zaidi ya muongo uliopita.
Lakini Angola ambayo idadi yake ya wakazi ni karibu milioni 26 ni ndogo ukilinganisha na jirani zake, inaamini kwamba maslahi yake yatakuwa salama ikiwa Congo itakuwa na utulivu, ingawa ni dhaifu na imekuwa ikiingilia kati kwa njia za kijeshi na kidiplomasia katika kipindi cha nyuma ili kuhakikisha kuwa hali ya usalama inadumishwa.
Mapema mwaka 1998 katika vita iliyodumu hadi 2003, ndege za kivita za Angola ziliwashambulia askari wa Rwanda waliokuwa wakielekea Kinshasa. Wakati vita ya bunduki ilipoibuka mji mkuu wa Kinshasa mwaka 2006, wanajeshi wa Angola walikwenda kuwasaidia walinzi wa Kabila kupambana na wapiganaji tiifu wa Jean-Pierre Bemba,(Jan Piyer Bemba) muasi wa zamani aliyeshindwa katika uchaguzi.
Lakini katika hali inayoashiria kwamba Angola inatatizwa na kile kinachoendelea nchini Congo, kama mwanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2015 na 2016, ilipiga kura ya maazimio makali dhidi ya Congo katika Umoja wa Mataifa.
Pia imeonyesha wasiwasi kwa kuweka shinikizo kwa Kabila ili akubali hatua ya pili ya majadiliano mwishoni mwa mwaka jana baada ya mazungumzo ya serikali ya mpito yaliyoratibiwa na Umoja wa Afrika wa kuwajumuisha viongozi wakuu wa upinzani kushindwa.
Mshauri wa juu wa masuala ya diplomasia wa Kabila anasema serikali ya Congo inaelewa wasiwasi wa Angola juu ya machafuko karibu na mpaka wake lakini akasema kwamba Angola haijaweka shinikizo katika siasa zake za ndani.
Mwandishi: Sylvia Mwehozi
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman