Angani na Astrium
4 Juni 2013Ikishika nafasi ya kwanza barani Ulaya na ya tatu ulimwenguni, Astrium inaajiri wanaume na wanawake wapatao 18,000 kutoka sehemu mbalimbali duniani. Wataalamu 18,000 waliochaguliwa miongoni mwa walio bora zaidi, wote wakiwa na shauku ya kuchunguza kinachojiri angani, wakisukumwa na uthubutu wa hali ya juu wa wakati wetu - ambao ni kuuleta duniani, uwezo usio na kikomo wa anga ili uwanufaishe wanaadamu.
Kufanya kazi Astrium
Kwa watu wengi, fani ya sayansi ni ngumu, na ugumu huu unaongezeka zaidi unapozungumzia masuala ya usafiri wa anga. Hata maelezo yanayotolewa na wataalamu hao kuhusiana na shughuli zao yanakuwa magumu kwa akili ya kawaida, jambo lililonisukuma kumuuliza Andreas Schütte, Mkurugenzi wa Programu ya Texus na Maxus kuhusu mtazamo wake yeye na wenzake kuhusiana na kazi wanazozifanya katika kituo chao kilichoko katika mji wa Bremen, Kaskazini-magharibi mwa Ujerumani.
"Nikiangalia kwa mfano watu waliomo katika timu yangu, wana motisha kubwa na wanafurahia sana kazi yao kiasi kwamba wengi wao wamekuwa wakifanya kazi katika programu hiyo tangu miaka 25 na hawajawahi kubadilisha kazi. Inavutia sana na wameendelea na programu hii ya Texus na hivi ndivyo ilivyo kwa programu nyingine. Ndiyo maana kuna utaalamu mkubwa sana hapa Astrium. Watu wanavutiwa sana na kazi zao, ni mashabiki w akweli wa anga, kama nilivyo mimi mwenyewe," anasema Schütte.
Ikiwa na jukumu la kuhakikisha kuwa bara la Ulaya linapata huduma zote zinazoweza kupatikana kutoka angani, kama kampuni inayoongoza katika usafiri wa anga, mifumo na huduma za satelaiti, Astrium imejifunga kwa kipindi cha miaka 40 iliyopita, kutoa huduma hizi kwa wakati uliyopo na ujao. Ni kazi ambayo inajihusisha na majina mengi ya kifahari katika anga - kama Kombora la Ariane, kituo cha kimataifa cha anga (ISS), Envisat, Mars Express na Skynet 5.
Biashara ya Astrium
Schütte anasema misheni ya Astrium ni yenye uthabiti, ikilenga kutoa ufumbuzi bora iwezekanvyo kwa mahitaji ya wateja kwa viwango bora zaidi, ufanisi wa gharama na kwa kuzingatia ratiba. Ubora wa kiufundi na uzoefu wa kampuni ya Astrium unakata katik sekta zote za biashara ya angani - ikiwa ni pamoja na uzinduzi wa magari, shughuli za angani zinazoendeshwa na wanaadamu, na mifumo ya sateliati na shughuli nyingine zinazohusiana na usafiri wa angani.
Astrium inajivunia kuwa na vifaa bora vya ubunifu, utengenezaji na majaribio katika sekta ya usafiri wa anga. Kampuni hiyo pia inajivunia mbinu za utaalamu wa juu na teknolojia zinazohitajika katika uendelezaji na uwasilishaji wa mifumo mikubwa ya angani. Wafanyakazi wa kampuni hiyo walio na motisha na uzoefu wa hali ya juu, wanahakikisha kuwa wanawapatia wateja wao - wawe wa kiraia, kijeshi, taifa, taasisi au kibiashara, suluhisho bora kwa mahitaji yao, wakijumuisha ubora, ufanisi wa gharama, uzingativu w amuda na ubunifu endelevu. Astrium inaendesha shughuli zake kupitia matawi matatu.
Usafiri wa anga, setilaiti na huduma za Astrium
Kampuni ya Astrium ndiyo mkandarasi mkuu wa usafiri wa angani wa kiraia na kijeshi katika bara la Ulaya. Inaunda, kuendeleza na kutengeneza mitambo ya kufyatulia roketi za Ariane na makombora ya masafa marefu kwa ajili ya kikosi cha Ufaransa cha kuzuiwa nyuklia. Pia ndiyo mkandarasi mkuu wa maabara ya Columbus, na chombo cha kusafirisha mizigo cha ATV kinachohudumia kituo cha usafiri wa anga, ISS.
Astrium inaongoza katika kubuni na kutengeneza mifumo ya setilaiti, ambapo shughuli zake za kibiashara zinajumuisha mawasiliano ya simu ya kiraia na kijeshi na uchunguzi wa ulimwengu, sayansi na mipango ya urambazaji, pamoja na miundombinu mbalimbali ya ardhini na vifaa vya angani. Ni sehemu ya kipekee katika soko la huduma za setilaiti duniani, ikiwa na uwezo na utaalamu uisiokifani katika mawasiliano salama, huduma za uchunguzi wa dunia na huduma za urambazaji.
Ushiriki wa Afrika
Ingawa Andreas Schütte anasema wapo waafrika wanaotoa mchango katika kufanikisha shughuli za Astrium, anakiri kuwa mchango wa Afrika katika suala zima la utafiti wa angani bado ni mdogo sana. "Wakati mwingine nadhani ni kwamba hakuna ufahamu juu ya umuhimu wa mambo yanayoendelea angani kwa manufaa ya mwanadamu katika bara bara la Afrika," anasema mtaalamu huyo. Lakini ansema hivi karibuni wamekuwa na mazungumzo na Afrika Kusini yenye lengo la kuunga mkono programu ya kurusha roketi inayojulikana kama "Sounding" nchini humo, akionyesha matumaini kuwa miaka michache ijayo, huenda kukawepo na ushiriki zaidi wa mataifa ya Afrika.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman