ANC yazindua kampeni ya uchaguzi wa bunge Afrika kusini
13 Januari 2019Ramaphosa aliwasilisha manifesto yenye kurasa 68 mbele ya mamia kwa maelfu ya waungaji mkono chama hicho katika mji wa mashariki wa Durban, akizindua miezi minne ya kampeni.
Chama cha African National Congress ANC, ambacho kimeitawala nchi hiyo tangu kumalizika kwa utawala wa kibaguzi miaka 25 iliyopita, kinatarajiwa kushinda uchaguzi huo licha ya kupungua kwa uungwaji mkono, migawanyiko ya ndani pamoja na uchumi usio na kasi ya ukuaji.
Chama cha marehemu Nelson Mandela kiliathirika kwa kupungua uungwaji wake mkono chini ya urais uliokumbwa na kashfa tele wa rais Jacob zuma, ambaye aliondolewa Februari mwaka jana baada ya kuwapo madarakani kwa miaka tisa.
"tunapaswa kukiri kwamba makosa yalifanyika," ramaphosa alisema, na kuongeza: "Baada ya kipindi cha shaka na hali ya sintofahamu, tumewasili katika wakati wa matumaini na ujenzi mpya.
"Uchaguzi wa mwaka 2019 unatoa fursa ya kurejesha taasisi zetu za kidemokrasia na kuirejesha nchi yetu katika njia ya mabadiliko, ukuaji wa uchumi na maendeleo."
Uchunguzi wa maoni
Katika uchunguzi wa maoni ya wapiga kura uliofanyika hivi karibuni na kundi la IPSOS umetabiri kwamba ANC inaweza kupata kiasi ya asilimia 61 katika uchaguzi wa bunge la taifa na majimbo.
Katika kiwango cha bunge la taifa , hali hiyo itakuwa sawa na jinsi chama hicho kilivyopata katika uchaguzi wa mwaka 2014, wakati kilipopata asilimia 62. Katika bunge la Afrika kusini, chama hicho ambacho kina wingi wa viti pia kina fursa ya kumchagua rais.
Ongezeko hilo la utabiri unatokana na kuteuliwa kwa rais ambaye ni mwanamageuzi mpenda biashara Cyril Ramaphosa baada ya wabunge wa ANC kumlazimisha Zuma kujiuzulu mnamo wakati kashfa za rushwa zikiongezeka.
Wanaharakati ambao walivalia nguo zenye rangi ya chama hicho za manjano na kijani waliujaza uwanja wa mpira wenye uwezo wa kuingiza zaidi ya watu 85,000 katika mji huo wa pwani kwa ajili ya uzinduzi huo na walishangiria kwa nguvu wakati rais wa zamani Zuma , ambaye anatoka katika eneo hilo, alipojiunga na kundi la wacheza ngoma katika jukwaa.
Katika tukio la kupendeza na lililojaa vifijo , dazeni kadha za wapanda pikipiki wakipepea bendera ya ANC , walizunguka katika uwanja huo , wakiendesha pikipiki zao huku wakishangiriwa na kupigiwa makofi.
Katika mpambano mkali wa ndani wa chama hicho, Ramaphosa alishinda mpambano wa kuwania madaraka na kumrithi Zuma, ambaye mgombea aliyempendelea alikuwa mke wake wa zamani.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Zainab Aziz