Amnesty yaituhumu Iran kwa kuwazuwilia wafungwa matibabu
12 Aprili 2022Ripoti hiyo ya Amnesty imekuja kufuatia visa kadhaa vilivyorekodiwa mwaka huu pekee vya wafungwa mashuhuri waliofariki wakiwa kizuizini kutokana na kile wanaharakati wanasema ni kushindwa kwa Iran kuwatibu ipasavyo magonjwa yao.
Wafungwa hao ni pamoja na mshairi na mtengenezaji filamu wa Iran Baktash Abtin ambaye alikufa mwezi Januari, baada ya kuambukizwa maradhi ya Covid-19, na Shokrollah Jebeli, raia wa Australia mwenye asili ya Irani aliekuwa na umri wa miaka 82, ambaye alikufa mwezi Machi baada ya matatizo kadhaa ya kiafya.
Amnesty imesema vifo hivyo vilivyotokana na kunyimwa kwa maksudi huduma za afya, ni sawa na kunyongwa bila ya haki wakati kushindwa kwa Iran kutoa uwajibikaji ni mfano mwingine wa kimfumo wa kutowaadhibu wakosaji.
Diana Eltahawy, naibu mkurugenzi wa kanda ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini wa Amnesty, amesema kutojali maisha ya binadamu kunakoonyeshwa na serikali ya Irani kumeyageuza magereza ya nchi hiyo kuwa chumba cha kusubiria kifo kwa wafungwa wagonjwa, ambako magonjwa yanayotibika yanasababisha vifo.
Soma pia:Amnesty: Zaidi ya waandamanaji 100 wameuwawa Iran
Eltahawy amesema vifo vinavyotokana na kunyimwa huduma ya afya kwa makusudi ni sawa na upokaji wa maisha kiholela, jambo ambalo ni ukiukwaji wa haki za binadamu chini ya sheria za kimataifa.
Amnesty imesema imethibitisha vifo vya korokoroni vya wanaume 92 na wanawake wanne kwenye magereza 30 katika majimbo 18 kote Iran, vilivyotokea katika mazingira kama hayo tangu Januari 2010, lakini ikaongeza kuwa visa hivi ni kielelezo tu na kwamba idadi halisi inaweza kuwa kubwa zaidi.
Ushahidi wa Amnesty
Shirika hilo limesema limekusanya maelezo juu ya namna maafisa wa magereza wanavyowanyima wafungwa huduma za afya za kutosha mara kwa mara, ikiwa ni pamoja na vipimo vya uchunguzi, uchunguzi wa mara kwa mara, na huduma baada ya upasuaji.
Limesema wafungwa 64 kati ya 96 walikufa gerezani badala ya hospitali. Katika idadi kubwa ya visa, wafungwa waliokufa walikuwa vijana au watu wenye umri wa kati.
Sehemu kubwa ya vifo hivyo vilitokea katika magereza ya kaskazini-magharibi mwa Iran yanayohifadhi wafungwa wengi kutoka jamii ya Wakurdi na Waazabajani walio wachache, na kusini mashariki mwa Iran ambako wafungwa wengi wao ni wa jamii ya wachache ya Baluch wa Iran.
Soma pia: Msako dhidi ya watetezi wa haki waendelezwa Iran
Abtin, 47, ambaye alikuwa amehukumiwa kuhusiana na mashtaka ya usalama wa kitaifa na alikuwa akitazamwa na wanaharakati kama mfungwa wa kisiasa, alikufa kutokana na Covid-19 takriban wiki sita baada ya kuonyesha dalili katika gereza la Evin la Tehran.
Kwa upande wa Jebeli, Amensty imesema alikufa baada ya kuteswa kwa zaidi ya miaka miwili na kunyimwa huduma ya kutosha ya matibabu kwa hali aliyokuwa nayo ikiwa ni pamoja na mawe kwenye figo, kiharusi, maumivu miguuni, shinikizo la damu na ngiri ya kitovu.
Chanzo: Amnesty International