Amnesty: Wanaharakati wanawake wanashambuliwa na kuuawa
29 Novemba 2019Shirika la kimataifa la Amnesty International limesema katika ripoti yake kwamba watetezi wa haki za binadamu mara nyingi wanapokea vitisho na mashambulizi ambayo yanahusiana na kazi yao ya kupigania haki za wanawake na usawa wa kijinsia.
Katika ripoti hiyo ya kuadhimisha siku ya kimataifa ya watetezi wa haki za wanawake, Amnesty imesema kwamba wanaharakati hao wameendelea kupokea vitisho, kudhulumiwa kingono, kudhalilishwa na hata kuuawa.
Katibu mkuu wa shirika hilo Kumi Naidoo amesema kuwa, "wanaharakati wa masuala ya haki za wanawake wanashambuliwa kwasababu ya kazi wanayoifanya. Vitisho hivi ni vikubwa kwa wale wanaokabiliwa na aina zote za unyanyasaji, kwa mfano ukiwa wewe ni mwanamke na unatoka jamii ya wachache, mtu wa makabila ya asili, maskini, unashiriki mapenzi ya jinsia moja basi unapaswa kupambana zaidi ili sauti yako isikike na wale walioko madarakani".
Licha ya maendeleo katika harakati za wanawake ambayo yamepata nguvu kuliko hapo awali, bado wanaharakati wa kike wanakabiliwa na shinikizo katika miaka ya hivi karibuni kutoka kwa wanasiasa, viongozi wa kidini na makundi yaliyo na vurugu yanayosambaza "siasa za kikatili".
Ripoti hiyo imepewa kichwa cha habari "Kukabiliana na mamlaka, kupinga ubaguzi; Wito wa hatua zaidi za kutambua na kuwalinda wanaharakati wa haki za wanawake". Ripoti hiyo imeitolea mfano nchi ya Poland ambayo baadhi ya wanaharakati wa kike wamekabiliwa na mashambulizi katika mazingira ambayo ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya wahamiaji vimeongezeka.
Kwingineko ikiwepo Bahrain na Misri, udhalilishaji kingono unatumika kama aina ya mateso ili kuwanyamazisha wanaharakati wa kike. Wanawake pia wanakabiliwa na ukatili wa majumbani na unyanyasaji kulingana na dhana za kimila ikiwemo vitisho vya talaka au kutenganishwa kwa nguvu na watoto wao. Vile vile wanaharakati wa wanawake mara nyingi wanakumbwa na kampeni za kupigia debe kushambulia tabia zao ambazo Amnesty wanasema zimeundwa makusudi ili kujenga uadui dhidi yao.
Mfano mzuri ni waziri wa zamani wa mambo ya ndani wa Italia Matteo Salvini ambaye alimdhihaki Carola Rackete, nahodha wa meli ya uokozi ya Sea-Watch 3, na kufuatiwa na wengine waliochochea unyanyasaji wa kijinsia na kulenga jinsia yake na mwonekano. Amnesty International inatoa wito wa wanawake hao kutambulika na kulindwa kutokana na kazi ya ujasiri wanayoifanya kuboresha maisha na hususan jamii zilizotengwa.