Amnesty: Waasi wametenda uhalifu Aleppo, Idlib
5 Julai 2016Shirika hilo lenye makao yake mjini London Uingereza, limeainisha visa 24 vya utekaji nyara uliyofanywa na makundi ya silaha katika mikoa ya Aleppo na Idlib kati ya 2012 na 2016. Waathirika walijumuisha wanaharakati wa amani na watoto, na vile vile watu wa jamii za wachache waliolengwa haasa kutokan na dini yao.
Shirika hilo limewanukuu wanaharakati wakisema kuwa vuguvugu la Nour al-Dine Zanki na kundi la Jabhatu Nusra lenye mafungamano na mtandao wa Al-Qaeda, pia yalitumia aina fulani ya mateso sawa na yanayofanywa na utawala wa rais Bashar al-Assad.
Miongoni mwa makundi ya waasi yalionyooshewa kidole kwa kufanya ukiukaji ni vuguvugu la Nour al-Dine Zanki, Levant Front, Divisheni ya 16, Ahrar al-Sham na Jabhatul Nusra. Taasisi ya Marekani ya utafiti wa vita ilisema katika ripoti iliyochapishwa mwezi Februari kuhusu makundi ya upinzani mjini Aleppo, kwamba makundi matatu ya kwanza yalikuwa wapokeaji wa sasa au wa zamani wa msaada wa Marekani.
Wakurd na Wakristu walengwa
Amnesty ilitolea mfano wa kisa cha "Halim," mfanyakazi wa misaada ya kiutu, alietekwa na vuguvugu la Nour al-Dine Julai 2014 wakati akisimamia mradi katika hospitali mjini Aleppo. Limesema mfanyakazi huyo alizuwiliwa mawasiliano kwa karibu miezi miwili kabla ya kulaazimishwa kuungama chini ya mateso.
Alisema alipokataa kusaini waraka wa kuungama mtu aliekuwa akimhoji alimuagiza mlinzi amtese. "Na hapo alianza kunipiga kwa kutumia nyaya kwenye visigino vyangu vya miguu, nilishindwa kuhumili mateso hivyo nikasaini karatasi," alisema Halim.
Amnesty ilisema wanachama wa kabila la wachache la Wakurdi katika wilaya ya Sheikh Maqsoud inayodhibitiwa na vikosi vya Wakurdi mkoani Aleppo, na pia mapadri wa Kikristu walilengwa katika utekaji nyara wa makundi ya waasi.
Walengwa wa makundi ya silaha, wanaanzia kwenye wanaharakati wa habari, waandishi wa habari, wafanyakazi wa mashirika ya kiutu, wanaharati wa kisiasa, na katika maeneo mengine watoto pia," alisema Philip Luther, mkurugenzi wa programu ya Mashariki ya Kati na Afrika Kaskzini wa Amnesty International.
"Na katika baadhi ya matukio, inaelekea walitekwa kwa sababu tu ya kukosoa utawala wa makundi ya silaha katika eneo lao. Na katika baadhi ya visa, inaonekana walilengwa kwa sababu ya kabila au dini yao. Hivyo katika baadhi ya visa walikuwa Wakurd waliolengwa na makundi hayo ya silaha."
Wafadhili waombwa waingilie kati
Luther alisema wakati baadhi ya raia katika maeneo yanayodhibitiwa na makundi ya silaha mwanzo walikaribisha kuondolewa katika utawala wa kikatili wa Bashar Assad, matumaini yao kwamba makundi hayo yangeheshimu haki zao yametofifia, kutokana na makundi hayo kuzidi kuchukulia sheria mikononi na kutenda ukiukaji mkubwa wa haki.
Amnesty imeyatolea mwito mataifa makubwa kuyashinikiza makundi ya silaha kukomesha ukiukaji huo na kuheshimu sheria za vita. Ripoti ya shirika hilo ilisema pia mataifa ya kanda yanapaswa kuacha kutoa silaha na aina nyingine za msaada kwa makundi yoyote yanayojihusisha na uhalifu wa kivita au ukiukaji mwingine.
Ilisema makundi yanayotuhumiwa yanaaminika kuungwa mkono na serikali kama vile Qatar, Saudi Arabia, Uturuki na Marekani.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/afpe,rtre
Mhariri: Mohammed Khelef