Vikosi vya Eritrea vyashutumiwa kufanya ukatili Tigray
5 Septemba 2023Shutuma hizo zimetolewa licha ya kuwepo makubaliano ya kusitisha mapigano.
Katika ripoti ya shirika hilo iliyochapishwa jana Jumatatu, Amnesty International imesema wanajeshi wa Eritrea wamewaua raia na kuwanyanyasa wengine kingono kwa miezi kadhaa baada ya kutiwa saini mkatabaa wa amani. Shirika hilo limesema matendo hayo yanayojumuisha ubakaji na uporaji mali yanakidhi kuwa jinai za kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Wanajeshi wa Ethiopia wanawarudisha nyuma wapiganaji wa Amhara
Shirika hilo limesema wafanyakazi wake wamezungumza na wanawake 11 waliosema wamebakwa au kufanywa watumwa wa ngono hata baada ya kupatikana makubaliano ya kukomesha uhasama kati ya vikosi vya ukombozi wa jimbo la Tigray na vile vya serikali kuu ya Ethiopia, Novemba mwaka jana.
Kwa miaka miwili pande hizo mbili zilitumbukia kwenye mapigano makali yaliyosababisha vifo vya mamia kwa maelfu ya watu na wengine wengi kupoteza maeneo yao ya kuishi. Kwenye mzozo huo vikosi vya taifa jirani la Eritrea vilipigana bega kwa bega na vile vya serikali ya Ethiopia.