1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIraq

Amnesty yaonya kuongezeka matumizi ya risasi za mpira

14 Machi 2023

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu, Amnesty International limeonya kuhusu kuongezeka kwa matumizi ya risasi za mpira zinazotumiwa na polisi dhidi ya maandamano ya amani ulimwenguni kote.

https://p.dw.com/p/4Odqi
Thailand APEC 2022 Gipfel Proteste Polizei
Picha: Wason Wanichakorn/AP Photo/picture alliance

Hayo yameelezwa katika ripoti ya shirika hilo lenye makao yake mjini London, Uingereza ambayo imetolewa Jumanne, na kwamba matumizi hayo ya risasi za mpira na silaha nyingine, dhidi ya watu wanaoandamana kwa amani yamesababisha wengi kupata majeraha ya macho na hata vifo.

Amnesty International imetoa wito wa kuwepo udhibiti bora wa kimataifa wa biashara na matumizi ya vifaa hivyo vya polisi, ambavyo pia vinajulikana kama "silaza zisizo na madhara makubwa".

Ripoti hiyo imetolewa baada ya shirika hilo kufanya utafiti kwenye zaidi ya nchi 30 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.

Waandamanaji wengi wamekuwa walemavu

Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyopewa jina "Jicho Langu Limelipuka", maelfu ya waandamanaji na watazamaji wamekuwa walemavu na wengine kadhaa wameuawa kutokana na uzembe wa matumizi mabaya na ya mara kwa mara ya silaha hizo katika kutekeleza sheria kandamiza dhidi ya maandamano ya amani.

Silaha hizo ni pamoja na risasi za mpira, vilipuzi vya mpira na mabomu ya kutoa machozi ambayo zilifyatuliwa moja kwa moja dhidi ya waandamanaji katika maeneo ya Amerika ya Kusini na Kati, Ulaya, Mashariki ya Kati, Afrika na Marekani.

Amnesty International imesema kumekuwa na ongezeko la kutisha la majeraha ya macho, ikiwa ni pamoja na kupasuka kwa mboni ya jicho, kuchanika kwa eneo la ndani ya jicho na watu kupoteza kabisa uwezo wa kuona.

Irak | Jahrestag Oktoberrevolution | Demonstration in Bagdad
Polisi wa Iraq, wakiwatawanya waandamanaji mjini Baghdad kwa mabomu ya kutoa machoziPicha: Murtadha Al-Sudani/AA/picture alliance

Nchini Chile pekee, kuanzia Oktoba mwaka 2019, kulikuwa na zaidi ya visa 30 vya watu kupoteza uwezo wa kuona baada ya polisi kukabiliana na waandamanaji. Hayo ni kwa mujibu wa Taasisi ya Kitaifa ya Haki za Binaadamu.

Ripoti hiyo imesema waandamanaji wengine kwenye nchi kadhaa zilizofanyiwa utafiti pia mifupa yao na mafuvu yalivunjwa, walipata majeraha ya ubongo, kupasuka kwa viungo vya ndani ya mwili na kupasuka kwa mbavu. Kwa mujibu wa ripoti hiyo iliyoandikwa kwa ushirikiano na Wakfu wa Utafiti wa Omega, waandamanaji wengine pia waliuawa.

Shirika hilo la kimataifa la kutetea haki za binaadamu limesema nchini Iraq, vikosi vya usalama vilifyatua kwa makusudi kabisa mabomu ambayo ni mazito mara 10 zaidi kuliko mabomu ya kawaida ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji, na kusababisha takribani vifo 24 mwaka 2019.

Sheria za kimataifa zinahitajika kuzuia ongezeko hilo

Nchini Uhispania, matumizi ya risasi zenye ukubwa wa mipira ya kuchezea mpira wa tennis yalisababisha kifo takribani kimoja kutokana na majeraha ya kichwa.

Hayo yameelezwa na shirika la Stop Balas de Goma, linalofanya kampeni ya kuzuia matumizi ya risasi za mpira.

Patrick Wilcken, mwanaharakati wa haki za binaadamu anayefanya kazi na Amnesty International anasema udhibiti unaofungamana na sheria ya kimataifa kuhusu kutengeneza na biashara ya silaha zisizo na madhara makubwa na zenye hatari pamoja na miongozo madhubuti ya matumizi ya nguvu, zinahitajika haraka ili kupambana na mazunguko unaoongezeka wa unyanyasaji.

 

(AFP)