Amnesty, Greenpeace wataka Trafigura ishitakiwe
25 Septemba 2012Cote d'Ívoire inasema kuwa sumu hizo ambazo zililetwa na meli inayoitwa Probo Koala chini ya usimamizi wa kampuni ya Trafigura zilisababisha vifo vya watu 17 na kuwaathiri wengine maelfu kiafya.
Ripori ya mashirika hayo yenye kurasa 250 inasema na hapa nainukuu kuwa " Serikali ya Uingereza ni lazima ianze uchunguzi wa kesi ya jinai kwa kampuni ya Trafigura kwa kitendo chake hicho cha kutupa sumu hizo kwa kuwa tawi la Kampuni hiyo la Uingereza ndilo lililoshirika kwa kaisi kikubwa katika kuzua janga hilo.
Trafigura yakana
Hata hivyo kampuni ya Trafigura ambayo makao yake yako nchini Uswis imekana kuwepo kwa uhusiano wowote baina ya sumu hizo na vifo vya watu hao 17 pamoja na madhara mengine yanayotajwa kuwapata binadamu kutokana nazo. Katika tamko la kampuni hiyo, Tragura imeikosoa ripoti ya mashirika hayo ikisema kuwa imerahisisha kupita kiasi masuala magumu ya kisheria.
Mwezi Julai mwaka 2006, mabaki ya madini aina ya Caustic Soda na mafuta ya petroli yakiwa yamepakiwa kwenye meli ya Probo Koala yalizuiwa kuingia kupakuliwa ili yaweze kuchujwa kwenye bandari ya Amsterdam na badala yake ylipelekwa mjini Abidjan ambako yalitupwa kwenye majalala ya mji huo.
Taka hizo zikiwa zimewekwa kwenye matanki ya kusafishia petroli inayotakiwa kusafishwa, yalirudishwa tena kwenye meli baada ya kugundulika kuwa ni hatari zaidi kuliko ilivyodhaniwa mara ya mwanzo na kampuni ya kuchuja sumu kwenye mabaki ya taka za kemikali ya Uholanzi ilitaka kiasi kikubwa cha pesa kufanya kazi hiyo. Kampuni ya Trafigura ilikataakulipa kiasi hicho cha fedha.
Amnesty International na Green Peace zinakikosoa kitendo hicho cha kuyarudisha melini matangi hayo ya sumu yakisema kuwa ni uvunjifu wa sheria za Uholanzi.
Katibu Mkuu wa Amnesty Salil Shetty anasema na hapa ninamkuu " Watu wa Abidjan wa walidhuriwa si na serikali yao bali na serikali zote za Ulaya ambazo hazikuhakikisha zinatumia sheria zao kuzuia kitendo kama hicho".
Mahakama nchini Uholanzi iliikuta kampuni ya Trafigura na makosa ya kusafirisha sumu kutoka nchi hiyo kinyume na sheria, lakini waendesha mashitaka hawakutilia maanani madhara yaliyoikumba Cote d´Ivoire baada ya kutupwa sumu hizo.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Green peace Kumi Naidoo anasema na ninamnukuu " Bado hatujachelewa kwa sheria kuchukua mkondo wake, kwa watu wa Abidjan kuelezwa hasa ni sumu gani zilitupwa na Trafigura ikawajibika kutokana na makosa yake. Kwa kufanya hivyo tu, ndio tunaweza kuzuia makosa ya aina hii kufanywa tena hapo siku za baadae"
Ripoti hiyo imeonyesha mashaka juu ya sheria za Cote d´Ivoire ambazo zinatoa mwanya kwa kampuni hiyo kukwepa mashataka yake kuendeshwa nchini humo na hivyo imetoa wito kwa serikali kuhakikisha waatihirika wote wa sumu hizo wanafidiwa kikamilifu.
Mwandishi: Stumai George/AFP
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman