Amerika Kusini yaigwaya Marekani kuhusu Snowden
3 Julai 2013Mtaalamu kutoka shirika la ushauri la Inter-Amercan Dialogue la mjini Washington, Micheal Shifter, anasema mataifa ya Amerika Kusini yana hisia zinazokinzana juu ya wakala huyo wa zamani wa upelelezi anaeaminika kukwaama katika uwanja wa ndege wa Moscow nchini Urusi, na ambae ameomba hifadhi ya kisiasa katika mataifa 21.
Hofu ya kukwaruzana na Marekani
Shifter anasema kwa upande mmoja kesi ya Snowden inatoa kishawishi kikubwa kwa mataifa kufanya jambo la kuipinga Marekani, kutuma ujumbe na kuonyesha undumilakuwili na unafiki uliopo mjini Washington. Lakini kwa upande wa pili, kuna tabia ya uyakinifu nchini Venzuela, Nicaragua, Bolivia au Cuba. Licha ya maneno mengi, viongozi wa mataifa hayo wanajaribu kuwa karibu na Marekani. Yapo mambo kadhaa muhimu yaliyo hatarini, na hawataki kuingia katika hatari ya kukwaruzana na Marekani.
Utawala mjini Washington umebainisha wazi kuwa nchi yoyote itayomchukuwa Snowden ijiandae kwa madhara makubwa, kama msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni Patrick Ventrell amekuwa akirejea katika siku za hivi karibuni. Wakati wa ziara yake mjini Moscow, rais wa venezuela Nicolas Maduro, alipendekeza kuwa Snowden awekwe chini ya ulinzi wa kimataifa. Hii inaashiria safari ndefu ya Caracas kumpatia hifadhi Snowden.
Licha ya mashambulizi ya maneno ya Maduro dhidi ya Marekani wakati wa uchaguzi uliyomalizika hivi karibuni kufuatia kifo cha mtangulizi wake Hugo Chavez, aliekuwa mpinzani mkubwa sana wa Marekani, tawala mjini Caracas na Washington zinachukua hatua za siri kuboresha uhusiano baina yao na kutafuta njia ya kurudisha mabalozi wao. Nchi hizo mbili hazina uwakilishi wa kibalozi baina yao tangu mwaka 2010.
Kurejeshwa kwa mabalozi kutakuwa na maslahi hasa kwa Venzuela, kwa mujibu wa vyanzo vilivyo na ufahamu juu ya mazungumzo kati ya waziri wa mambo ya kigeni wa Venezuela Elias Jaua, na mwenzake wa Marekani John Kerry, yaliyofanyika wakati wa mkutano wa baraza kuu la umoja wa mataifa ya Amerika OAS mwezi Juni.
Ecuador yanyamanzishwa
Rais wa Ecuador Rafael Correa, ambae alisema wiki moja iliyopita kuwa utawala mjini Quito ulikuwa unatafakari juu ya maombi ya Snowden ya hifadhi, pia amepunguza makali ya matamshi yake, baada ya mazungumzo ya kirafiki kwa njia ya simu na makamu wa rais wa Marekani, Joe Biden mwishoni mwa wiki.
Tayari Equador itapoteza upendeleo wa kibiashara ambao bunge la Marekani lingerefusha muda wake mwishoni mwa mwezi huu wa Julai. Uamuzi huo unaaminika kuchukuliwa hata kabla Snowden hajaomba hifadhi nchini Equador. Lakini baadhi ya wabunge wa Marekani wameitumia kesi hiyo kuikumbusha Equardor juu ya ukubwa wa hasara ya kiuchumi inayoikabili.
Viongozi wamataifa ya Amerika Kusini ambayo yangeshawishika kumkubali Snowden, wanatka kuendelea kuwepo madarakni, na kuendelea kuwepo wanahitaji nafuu ya kiuchumi, na kwa namna yoyote ile, Marekani inaendelea kuwa mshirika muhimu zaidi, hata kama siyo mdau pekee, alisema Shifter, na kuongeza kuwa wote viongozi hao wanapima yote hayo.
Njia ndefu kwa Snowden
Cuba nayo inapima faida na madhara ya kumpa hifadhi Snowden, na matokeo siyo mazuri sana kwa mtotro huyo wa kimataifa. Cuba inajiandaa kuanza tena majadiliano na Marekani, juu ya suala tete linalohusiana na uhamiaji, na inajaribu kuishawishi Marekani iondoe katika orodha ya mataifa yanayowalinda magaidi duniani.
Mataifa yanayotafakari kumpa hifadhi Snowden pia yanakabiliwa na kikwazo kingine. Msimamo wa pamoja dhidi ya mvujishaji huyo, ambao unakata pande zote za kisiasa nchini Marekani. Shifter anasema iwapo serikaliza mataifa hayo zitajaribu kumpa hifadhi Snowden, basi hazitapata washirika, hasa kutoka nyanja ya siasa.
Mwandishi: Iddi Ismail Ssessanga/dpae
Mhariri: Josephat Charo