1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aleppo Mashariki wajiandaa kwa mashambulizi mapya

5 Novemba 2016

Waasi wa Syria na raia hawakuonyesha ishara ya kuondoka katika eneo lililozingirwa mashariki mwa mkoa wa Aleppo siku ya Ijumaa, licha ya makataa ya Urusi kurejea mashambulizi mkoani humo baada ya usitishaji wa siku 17.

https://p.dw.com/p/2SCL7
Syrien Kämpfe in Aleppo
Picha: picture alliance/abaca/B. el Halabi

Mashambulizi ya waasi katika maeneo ya wakaazi ya upande wa Aleppo unaodhibtiwa na serikali uliuwa dazeni kadhaa katika kipindi cha wiki iliyopita, wakati waasi walipoanzisha mashambulizi ya kujibu kutokea nje ya mji huo wakilenga kuvunja mzingiro wa maeneo wanayoyadhibiti. Serikali ilituma magari ya kubebea wagonjwa na mabasi kuwaondoa watu katika ukanda uliozingirwa kama ilivyofanya huko nyuma wakati wa usitishaji mapigano, lakini bado hakukuwa na ishara kwamba kuna yeyote ambaye angeondoka.

Wakaazi waliowasiliana na shirika la habari la Reuters walionekana kuwa tayari kwa urejeaji wa mashambulizi, ambayo yaliuwa mamia ya watu mwishoni mwa mwezi Septemba na mwanzoni mwa Oktoba, wakati serikali na washirika wake wa Urusi walipoweka kando mpango wa kusitisha mashambulizi dhidi ya eneo kubwa zaidi la mjini lililoko mikononi mwa wapinzani.

"Hakuna kinachoweza kufanywa. Hakuna mtu anaweza kuzizuwia ndege," alisema Barbars Mishal, afisa wa shirika la ulinzi wa raia la 'White Helmets' katika Aleppo Mashariki, ambalo linafukuwa vifusi kuwatoa wahanga wa mashambulizi na kuendesha huduma ya magari ya kusafirisha wagonjwa. Moscow na Damascus zilisema mapngo wao wa usitishaji mapigano ungetimia saa moja jioni, na kuwatuhumu waasi kwa kutumia muda huo kuimarisha mashambulizi dhidi ya maeneo yanayodhibitiwa na serikali.

'Waasi ndiyo wa kulaumiwa'

Serikali ya Syria na washirika wao Urusi wanasema wanawalenga wapiganaji tu, na kwamba wapiganaji ndio wa kulaumiwa kwa vifo vya raia kwa kuendesha harakati zao katika maeneo ya kiraia. Mataifa ya Magharibi yanasema mashambulizi ya Syria na Urusi yamelenga kwa maksudi hospitali, wafanyakazi wa misaada na maduka ya kuoka mikate na serikali ya Marekani imeituhumu Moscow kwa "uhalifu wa kivita". Waasi wanasema lengo ni kuwaondoa raia, ambao 275,000 kati yao wanaendelea kuishi katika eneo lililozingirwa.

Wapiganaji wa kundi la Jabhat Fatah al Sham wakihudhuria mafunzo katika eneo la waasi lililozingirwa Aleppo Oktoba 26, 2016.
Wapiganaji wa kundi la Jabhat Fatah al Sham wakihudhuria mafunzo katika eneo la waasi lililozingirwa Aleppo Oktoba 26, 2016.Picha: Reuters/A. Ismail

"Wanauita usitishaji mapigano. Utawala haujaturuhusu kusikia mwisho wake," alisema Modar Shekho, muuguzi alieko katika la waasi mashariki mwa Aleppo. "Kama kawaida, unapoisha wataanza kufanya mashambulizi mara moja. Tumeshazowea." Jeshi la Syria, likiungwa mkono na wapiganaji wa Kishia kutoka Lebanon, Iran na Iraq, lilianzisha mashambulizi makubwa kurejesha udhibiti wa eneo la Aleppo Mashariki kutoka kwa waasi Septemba 22, baada ya kufanikiwa kuuzingira katika kipindi cha majira ya joto mwaka huu.

Aleppo imekuwa kitovu cha mapigano katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Syria, vilivyoingia katika mwaka wake wa sita sasa, vikimpambanisha rais Bashar al-Assad na washirika wake dhidi ya makundi ya waasi wa madhehebu ya Sunni, yakiwemo baadhi yanayoungwa mkono na Uturuki, mataifa ya Ghuba na Marekani.

Mji huo umegawanyika kati ya eneo la magharibi linalodhibitiwa na serikali, na upande wa mashariki unaodhibitiwa na waasi kwa miaka kadhaa. Kupata udhibiti kamili wa Aleppo ungekuwa ushindi mkubwa zaidi kwa serikali ya Assad, katika vita ambavyo vimeuwa mamia kwa maelfu ya watu na kuwalaazimu zaidi ya nusu ya Wasyria kuyakimbia makaazi yao.

"Hakuna atakaeondoa"

Damascus na Moscow zilitangaza mpango wa upande mmoja wa kusitisha mapishambulizi Okotoba 18, wakiwaahidi waasi na raia njia salama kuondoka mjini humo, na wameurefusha mpango huo kwa siku zaidi tangu wakati huo, ingawa kumekuwa kukifanya mashambulizi baadhi ya wakati. Urusi ambayo imepeleka meli ya ziada ya kubebea ndege katika pwani ya Syria, ilisema siku ya Jumatano kwamba waasi wote wanapaswa kuondoa Aleppo kufikia Ijumaa jioni, na kuongeza kuwa uzuwiaji wake wa mashambulizi haungeweza kurefushwa kutokana na mashambulizi ya waasi.

Russischer Flugzeugträger Admiral Kusnezow
Urusi imetuma meli yake ya kivita iitwayo Admiral Kuznetsov katika pwani ya Syria kuimarisha mashambulizi dhidi ya waasi mkoani Aleppo.Picha: picture-alliance/PA Wire/G. Fuller

Shuhuda moja Aleppo Magharibi, katika eneo la Bustan al-Qasri, karibu na kivuko kilichowekwa na serikali kuwaruhusu raia kuondoka katika maeneo ya waasi, aliliambia shirika la habari la Reuters siku ya Ijumaa kwamba hakuona watu wanaowasubiri ndugu wanaokuja kutokea upande wa Mashariki. Mabasi na gari za wagonjwa vilikuwa vinawasubiri, lakini hakukuwa na ishara ya uhamaji.

Mwanamke katika Bustan al-Qasr aliekuwa amefunika uso wake alisema alitumaini watu mashariki mwa Aleppo wangeweza kuondoka salama na kwa amani. Lakini waasi wanakataa takwa la kuwataka waondoke. "Hakuna atakaeondoka na Warusi wataongeza tu. Warusi walishatangaza hili," alisema Zakaria Malahifji, afisa alieko nchini Uturuki wa kamati ya kisiasa ya kundi la Fastaqim, ambalo lina uwakilishi mjini Aleppo.

Wapinzani wanasema Damascus na washirika wake wa Urusi na Iran wanalenga kushinda vita kwa kuondoa wakaazi katika maeneo yanayoshikiwa na waasi, kuwauwa kwa njaa au kuwapiga mabomu hadi wakimbie. " Warusi wanatumia sera ya mabadiliko ya demografia kwa pamoja na utawala na Iran, na nia yao haifichiki tena," alisema afisa kutoka kundi la waasi la Nouri al-Dine al-Zinki.

Mkakati wa utawala wa Assad na Urusi

Katika miezi ya karibuni maeneo yanayodhibtiwa na waasi yamejisalimisha baada ya mizingiro ya muda mrefu. Serikali inautaja mchakato huo kuwa ni maridhiano, ikitoa njia salama kwa wapiganaji wa makundi ya waasi wanaoondoka na kuweka chini silaha zao. Imependekeza mpango sawa na huo ili kukomesha mzingiro wa Aleppo Mashariki, ikifungua kile ambacho jeshi linakitaja kuwa njia salama, na kutuma magari ya wagonjwa kwa ajili ya majeruhi na mabasi kusafirisha wapiganaji kwenda Idlib, ambalo ni eneo la waasi.

Lakini mpaka sasa idadi ndogo tu ya watu wameondoka katika ukanda unaoshikiliwa na waasi tangu mwezi Oktoba. Damascus imewatuhumu waasi kwa kuwazuwia watu kuondoka, ikiwemo kwa kuzishambulia njia salama, tuhuma ambazo waasi wamezikanusha.

Syrien Rebellenkämpfer
Wapiganaji wa upande wa waasi wakiendesha kifaru katika kiunga cha Dahiyat al-Assad walichokiteka magharibi mwa Aleppo Oktoba 28,2016.Picha: Reuters/A. Abdullah

"Natamani raia wangetoka...lakini nataraji hilo halitatokea, si katika mazingira haya," alisema  Fadi Ismail, afisa wa wizara ya maridhiano ya Syria alieko mkoani Aleppo akizungumza na shirika la reuters kwa njia ya simu. Ismail alisema matarajio y akufikia makubaliano na waasi yanaonekana kuwa madogo sana. "Bila shaka laazima kuwepo na hatua za kijeshi," alisema, iwapo hakuna atakaendolewa.

Umoja wa Mataifa wapinga

Umoja wa Mataifa umesema hauna uhakikisho wa kiusalama unalohitajika kufikisha misaada ya kiutu mashariki mwa Aleppo. Unapinga kuondolewa kwa raia kutoka maeneo yaliozingirwa isipokuwa kama ni wa hiari. Baada ya mashambulizi kuanza mwishoni mwa mwezi Septemba, vikosi vitiifu kwa serikali vilifanikiwa kupata mafanikio kaskazini mwa Aleppo, ikiwemo kambi ya wakimbizi wa Kipalestina na maeneo madogo ya kusini, lakini hakujawa na hatua kubwa katika maeneo yalio na wakaazi wengi.

Waasi walifanya mashambulizi ya kujibu katika kingo ya magharibi ya maeneo yanayodhibitiwa na serikali kutokea pembezoni. Wamepata mafanikio katika kiunga cha Dahiyet al-Assad na wilaya yenye majengo 1070, wakitumia mashambulizi 15 ya magari ya kujitoa muhanga katikati mwa wiki, alismea mfuatiliaji mmoja wa vita. Shirika la uangalizi wa haki za binaadamu la Syria lilisema waasi waliuwa raia 69 wakiwemo watoto 25 katika mashambulizi ya kujibu.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre

Mhariri: Bruce Amani