Albino mwingine akatwa mkono Tanzania
17 Februari 2013Washambuliaji wanaokusanya viungo vya mwili vya watu wenye ulemavu wa ngozi, (Albino) kwa ajili ya itikadi za kishirikina wamemkata mkono kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 7 nchini Tanzania, ikiwa ni tukio la hivi karibuni kabisa katika mfululizo wa mashambulizi ya kinyama dhidi ya watu hao.
Taarifa hizo zimetolewa leo Jumapili na maafisa nchini Tanzania.Kijana huyo Mwigulu Magessa ambaye yuko Hospitali kwa sasa alikatwa mkono wake Jumamosi usiku katika wilaya ya Milepa iliyoko Kusini Magharibi ya Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa za afisa wa serikali katika eneo hilo, Apolinary Macheta, kijana huyo alishambuliwa na watu watatu wakati alipokuwa akitembea kuelekea nyumbani kwao akiwa pamoja na marafiki zake wanne wakitokea shule.
Imani za kishirikina
Tukio hilo limefanyika siku kadhaa baada ya mwanamke mmoja mwenye ulemavu huo wa ngozi na mama wa watoto wanne aliponyofolewa mkono wake na watu waliokuwa na mapanga. Polisi inasema wameshawakamata watu watano kufuatia tukio hilo baada ya kugundua mkono huo uliokuwa unaoza ukiwa umefichwa kwenye shamba.
Nchini Tanzania watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi wanauwawa na kutengwa kufuatia fikra potovu za kishirikina zilizoenea kwamba viuongo vya mwili vya watu hao vinaleta bahati na utajiri kupitia shughuli za kichawi. Kimsingi ulemavu huo wa ngozi unatokana na hitilafu za kinasaba zinazohusishwa na upungufu wa seli za Melanin zinazotengeneza rangi ya ngozi,nywele na macho kwa ajili ya kuvikinga dhidi ya miale ya jua.
Watu wenye ulemavu huo wanakabiliwa na hali ya kutengwa pamoja na kuwa katika hatari ya kuuwawa katika nchi nyingi za Kiafrika.
Itakumbukwa kwamba mwezi wa Januari mtoto mmoja aliyekuwa albino alifariki katika mkoa wa Tabora baada ya wachambuliaji kumkata mkono wake kwa kutumia panga. Kijo Bisimba kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu nchini Tanzania amesema kwamba mashambulio hayo yanaongezeka kwa kiasi cha kushtusha hali ambayo inazusha tena wasiwasi mpya baada ya miezi kadhaa ya utulivu.
Mauaji ya aina hiyo ya kishirikiana yamekuwa pia yakitokea katika nchi jirani ya Burundi na baadhi ya washambuliaji wanashukiwa kutokea nchini Tanzania ambako viuongo vya maalbino vinaweza kumletea mtu maelfu ya dola.
Mwandishi:Saumu Mwasimba
Mhariri:Bruce Amani