1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Sisi aapa kuuangamiza Udugu wa Kiislamu

6 Mei 2014

Mkuu wa zamani wa Jeshi la Misri Abdel Fattah al-Sisi ambaye kwa wakati huu ni mgombea wa Urais, amesema kundi la Udugu wa Kiislamu halitakuwepo nchini humo iwapo atachaguliwa kuiongoza.

https://p.dw.com/p/1BuML
Abdel Fattah al-Sisi, mkuu wa jeshi wa Zamani wa Misri ambaye kwa sasa anagombea urais
Abdel Fattah al-Sisi, mkuu wa jeshi wa Zamani wa Misri ambaye kwa sasa anagombea uraisPicha: Reuters

Hayo al-Sisi ameyasema katika mahojiano na vituo viwili binafsi vya televisheni CBC na ONTV ambayo yalirushwa jana jioni. Mtu huyoi ambaye anatarajiwa kupata ushindi katika uchaguzi wa baadaye mwezi huu, amesema kamwe Udugu wa Kiislamu hautaibuka tena na kuushutumu kutumia makundi ya wanamgambo kuiyumbisha nchi. Kiongozi huyo amesema kurejesha usalama ndani ya Misri na kuukarabati uchumi ndio masuala yatakayokuwa yenye kipaumbele kwake.

Kauli yake hiyo imechukuliwa kama kuondoa uwezekano wa kutafuta maridhiano ya kisiasa na kundi hilo ambalo ndilo lilikuwa lenye nguvu kubwa kisiasa nchini Misri, kabla ya mapinduzi yaliyomuondoa madarakani rais Mohammed Mursi ambaye ni mwanachama wa kundi hilo.

Msingi wa chuki ya umma

Al-Sisi anaonekana kujenga hoja zake juu ya msingi wa chuki ya umma dhidi ya Udugu wa Kiislamu baada ya kuchukua hatamu za uongozi miaka mitatu iliyopita, na matamshi yake yameashiria nia yake kuliangamiza kundi hilo ambalo limekuwepo kwa muda wa miaka 86. Abdelfatah al-Sisi alisema ni wananchi wa Misri walioliangusha kundi hilo, sio yeye.

Viongozi wengi wa Udugu wa Kiislamu akiwemo Mohammed Mursi wamewekwa gerezani
Viongozi wengi wa Udugu wa Kiislamu akiwemo Mohammed Mursi wamewekwa gerezaniPicha: AFP/Getty Images

''Mimi siyo niliyowanyamazisha udugu wa kiislamu bali ni wananchi wa Msiri. Siyo wajibu wangu kulishughulikia suala hilo bali huo ni wajibu wa watu wa Misri. Kundi hilo siyo la waislamu wa kweli na halina haki.'' Alisema na kuongeza kuwa kuwepo kwa kundi hilo lazima kungelisababisha mgongano na wananchi. Alisema anaheshimu katiba na iwapo asingefanya hivyo basi angekuwa hajiheshimu yeyei mwenyewe.

Alipoulizwa iwapo kundi la Udugu wa Kiislamu halitakuwepo nchini Misri atakapochaguliwa kuiongoza nchi, al-Sisi alijibu, ...Naam, halitakuwepo.

Hujuma dhidi ya taifa

Mgombea huyo wa urais amesema Udugu wa Kiislamu umekuwa ukiyatumia makundi ya wanamgambo kupigana vita kichinichini, huku wenyewe ukijitenga mbali na shutuma za mashambulizi, na kuongeza alipotaka kumuondoa madarakani Mohammed Mursi, baadhi ya maafisa wa kundi hilo walimuonya kuwa akifanya hivyo wanamgambo wa kiislamu kutoka Afghanistan na kwingine watakuja kupigana nchini Misri.

Abdel al-Sisi anatarajiwa kuushinda kirahisi uchaguzi wa rais baadaye mwezi huu wa Mei
Abdel al-Sisi anatarajiwa kuushinda kirahisi uchaguzi wa rais baadaye mwezi huu wa MeiPicha: REUTERS

Katika mahojiano hayo Abdel Fattah al-Sisi aliwataka wamisri kuunga mkono polisi na jeshi katika mapambano dhidi ya ugaidi. Aliahidi kushughulikia maombi ya polisi kuongezewa uwezo ili iweze kukabiliana vilivyo na visa vya ghasia , na kuongeza kuwa jeshi litakuwa tayari kusaidiana na polisi katika majukumu hayo.

Aidha, al-Sisi aliunga mkono sheria inayozuia maandamano, akisema ilikuwa lazima ili kuepusha vurugu zaidi. Hata hivyo amesema polisi itatoa kibali kwa wale wanaotaka kuandamana kwa amani.

Alisema, '' Tunazungumzia hapa nchi ambayo ilikuwa inaharibika. Watu wanapaswa kuelewa hali hii na kutuunga mkono. Anayefikiria vinginevyo, anataka tu kuihujumu Misri, na hatutaruhusu hilo''.

Katika mtaa mmoja, watu wanaomuunga mkono al-Sisi waliyaonyesha mahojiano ya kiongozi huyo katika migahawa, na makundi ya watu yalikusanyika kutazama. Wakati wa mapumziko na matangazo ya biashara, walishangilia na kuzipigia makofi nyimbo za kijeshi.

Shabiki mmoja wa kiongozi huyo, Alia el-Sayed Saad, alisema baada ya Mungu anamuabudu Abdel Fattah al-Sisi. ''Sisi siyo wajinga, tunaijua tofauti kati ya mtu mwadilifu na mwenye nia mbaya'', alisema mzee huyo wa miaka 65.

Mwandishi: Daniel Gakuba/APE/RTRE

Mhariri: Iddi Ssessanga