Al-Shabaab yashambulia kambi za jeshi na kuwaua watu 25
8 Juni 2024Watu wasiopungua 25 wameuawa katika mashambulizi ya kigaidi katika kambi nne za kijeshi katikati mwa Somalia. Msemaji wa jeshi la Somalia, Abukar Mohamed Hassan amelieleza shirika la habari la DPA kwamba, kundi la Al-Shabaabndio limehusika na mashambulizi hayo katika wilaya ya Eldheer.
Amesema vikosi vya jeshi lake, vilipambana vikali na wanamgambo wa kundi hilo na kulizuia kuchukua udhibiti wa wilaya na kwamba wamewaua magaidi 20. Wanajeshi wawili wa Somalia na wapiganaji watatu wanaoshirikiana na jeshi wameuawa katika makabiliano hayo ya leo.
Kulingana na msemaji huyo, washirika wa kimataifa wa Somalia walitoa usaidizi wa anga kwa jeshi la nchi hiyo. Ingawa hakutaja majina ya nchi hizo, lakini Uturuki na Marekani ndio zimekuwa zikitoa msaada wa mara kwa mara kwa jeshi la Somalia.