Al-Gore na tume ya IPCC ndio washindi wa tuzo ya amani ya Nobel 2007
12 Oktoba 2007Akitangaza uamuzi huo mwenyekiti wa kamati ya Nobel ya Norway Ole Danlbolt Mjoes alisema
‘’Wametunukiwa tunzo hiyo kwa juhudi zao za kuuhamasisha ulimwengu juu ya mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na binadamu na pia kuweka misingi ya hatua zinazohitajika kuchukuliwa kukabiliana na hali hiyo.’’
Al Gore aliyekuwa makamu wa rais wa Marekani katika utawala wa Bill Clinton na kushindwa katika kinyang’anyiro cha kuingia ikulu ya White House mwaka 2000 amejihusisha zaidi katika miaka ya hivi karibuni katika vita dhidi ya mabadiliko ya hali ya hewa.
Aliandaa filamu inayoangazia athari za mabadiliko ya hali ya hewa mwaka 2006 ‘’An Inconvenient Truth’’yaani ukweli unaokera ambayo iliimpa ushindi wa tunzo ya Oscar.Kupitia filamu hiyo Al Gore anasema.
Tunaweza kuzuia madhara makubwa yasitokee lakini ikiwa hatutachukua hatua za haraka basi kitisho hiki kitakuwa kikubwa kwa binadamu ambacho hatujawahi kukiona.Kwa hivyo ni lazima tuchukue hatua na nafikiri kwa kutumia utaalamu na uwezo wangu nilioupata katika kazi niliyokuwa nikifanya ninaweza kulenga kubadili mawazo ya watu juu ya ukweli huu.
Tume ya Umoja wa mataifa ya IPCC inayowajumuisha kiasi cha wanasayansi wa hali ya hewa 3000,watalaamu wa masuala ya baharini, wale wenye ujuzi wa mambo yanayohusu barafu wanauchumi na wataalamu wengine ni halmashauri ya juu duniani ya wanasayansi wanaoshughulikia suala la ongezeko la ujoto duniani na madhara yake.
Uamuzi wa Kamati ya Nobel wa kutoa tunzo hiyo ya amani kwa wanaharakati wa mazingira unaonyesha jinsi gani kamati hiyo inavyoendeleza kuangazia suala la mabadiliko ya hali ya hewa tafauti na desturi yake ambapo tunzo hiyo ilikuwa ikiwaendea wanaojihusisha zaidi na harakati za kuzuia mizozo na kuweka maazimio pamoja na kufanikisha shughuli za kuwapokonya watu silaha.
Kwa miaka mingi washindi watunzo hiyo wamekuwa wakipewa watu wanaotoa michango katika masuala ya misaada ya kiutu na kutetea haki za binadamu,na hivi karibuni tunzo hiyo imekuwa ikipata wanaharakati wa mazingira.Mwaka 2002 ilitunukiwa mkenya wangari Maathai mwanaharakati wa mazingira.Na mwaka jana Mohammed Yunus pamoja na washirika wenzake katika benki ya Grameen huko Bangladesh walipata tunzo hiyo kwa juhudi zao za kupambana na umaskini.
Baada ya kutangazwa mshindi wa mwaka huu,Al Gore makamu wa zamani wa rais wa Marekani alisema,Tunakabiliwa na hatari kubwa katika sayari hii.
Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa akizungumzia ushindi wa bwana al Gore amesema uamuzi huo unaonyesha ukweli wa mambo kwamba bila ya shaka mabadiliko ya hali ya hewa yanauathiri ulimwengu.
Washindi wa tunzo hiyo ya mwaka huu watapokea medali ya dhahabu,cheti cha Diploma na kugawana kitita cha dolla millioni 1.53.
Sherehe rasmi za kutolewa zawadi hizo itafanyika mjini Oslo Desemba 10.