Al Gore leo kupokea tuzo ya Amani ya Nobel
10 Desemba 2007OSLO
Makamo wa Rais wa zamani wa Marekani Al Gore na mwanasayansi mkuu wa jopo la hali ya hewa la Umoja wa Mataifa leo wanatarajiwa kupokea Tuzo ya Amani ya Nobel mjini Oslo Norway.
Wanatunukiwa tuzo hiyo kwa kutahadharisha dunia juu ya kile makamo huyo wa rais wa zamani wa Marekani alichokiita hali ya hatari ya kuongezeka kwa kiwango cha ujoto duniani.
Akizungumza katika mkesha wa kupokea tuzo hiyo mjini Oslo hapo jana Al Gore amesema kwamba kupunguza utowaji wa gesi za carbon dioxide zenye kuathiri mazingira ni muhimu sana kwa manusura ya ustaarabu duniani.
Al Gore anashirikiana tuzo ya Nobel ya Amani na Jopo la kiserikali la Umoja wa Mataifa juu ya mabadiliko ya hali ya hewa ambalo litawakilishwa katika sherehe za kutunukiwa tuzo hiyo mjini Oslo na kiongozi wake Rajenda Pachauri.
Tuzo nyengine za Nobel katika madawa,kemia,phyzikia,fasihi na uchumi zitatolewa kwenye sherehe tafauti mjini Stockholm Sweden.