1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Ahly mabingwa wa Afrika

18 Julai 2021

Klabu ya Misri Al Ahly imeendeleza rekodi ya ushindi mara 10 wa Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuicharaza Kaizer Chiefs ya Afrika kusini mabao 3-0.

https://p.dw.com/p/3wdX2
Fußball Klub-WM | Al-Ahly - Palmeiras
Picha: Karim Jaafar/AFP/Getty Images

Ushindi huu ni wa kihistoria kwa Ahly, ambayo imekua klabu ya kwanza kushinda taji hili mara mara tatu mfululizo.

Mohammed Sherif alifunga bao la ufunguzi kunako dakika ya 53, bao lake la sita katika michuano hiyo. Dakika ya 64 Mohammed 'Afsha' Magdy aliodoa shaka ya uwezekano wa kubeba ubingwa kwa kupachika wavuni bao la pili. Soma Al Ahly ndio mabingwa wapya wa vilabu Afrika

Mchezaji Amr el Sulaya aligongelea msumari wa mwisho kwa kupachika wavuni bao maridadi kwa kisigino dakika ya 74 ya mchezo na kumuacha hoi mlinda lango wa Kaizer Chiefs kutoka Nigeria Daniel Akpeyi.

Katika kipindi cha kwanza Kaizer walitapatapa sana na mambo yaliharibika zaidi wakati mchezaji Happy Mashiane alipoonyeshwa kadi nyekundu baada ya kumchezea sivyo beki Ahmed Tawfik. somaKombe la Klabu bingwa Afrika 

Kocha wa Al Ahly, mzaliwa wa Afrika Kusini, Pitso Mosimane, ambaye aliishabikia Kaizer Chiefs akiwa mtoto, amekua kocha wa kwanza Mwafrika kushinda mashindano hayo mara tatu.

Mosimane alifanikiwa mnamo 2016 akiwa na kilabu cha Afrika Kusini Mamelodi Sundowns, na msimu uliopita alishinda akiwa na klabu ya Ahly kwenye fainali ya Wamisri dhidi ya wapinzani Zamalek.

Ägypten Fußball Al-Ahly vs Zamalek
Picha: picture-alliance/Photoshot

Ahly wametia kibindoni $ 2.5 milioni kwa kushinda Ligi ya Mabingwa na wamehakikishiwa angalau dola milioni nyingine 3.5 watakaposhiriki Kombe la Dunia la FIFA huko Japan.

Kabla ya kusafiri kwenda Mashariki ya Mbali, klabu hii ya Misri ambacho imetwaa mataji 22 ya Afrika itacheza na washindi wa Kombe la Shirikisho la CAF Raja Casablanca wa Morocco katika mechi moja ya Kombe la CAF Super Cup.

 

Chanzo:/AFP