Akufo-Addo kuapishwa kuwa rais wa Ghana
7 Januari 2017Mwanasheria huyo wa zamani wa haki za binadamu mwenye umri wa miaka 72 ataapishwa kuchukua wadhifa wa urais katika sherehe itakayofanyika katika uwanja wa uhuru katikati ya jiji la Accra mbele ya wageni waalikwa 6,000 pamoja na wananchi wa kawaida.
Kiasi ya viongozi wa nchi 11 kutoka barani Afrika wanatarajiwa kuhudhuria, pamoja na rais anayeondoka madarakani , na marais wa zamani Jerry Rawlings na John Kufuor.
Polisi katika mji mkuu wameahidi kuweka ulinzi mkali katika sherehe hizo za kuapishwa, ambapo barabara kuu ndani na nje ya eneo la shughuli zitafungwa.
Wafanyabiashara tayari wameweka vibanda vyao vya biashara karibu wakiwa na matumaini ya kufaidika na sherehe hiyo kwa kuuza bendera za Ghana na vitu vingine kutoka katika chama cha Akufo-Addo cha New Patriotic.
Ghana mhimili wa uthabiti
Ushindi wa Akufo-Addo katika uchaguzi, pamoja na kipindi cha mpito kwa amani cha kubadilishana madaraka -- kinaimarisha nafasi ya Ghana kuwa mhimili wa uthabiti katika eneo hilo ambalo mara kwa mara huwa linakumbwa na machafuko.
Mdadisi mmoja wa masuala ya kisiasa wa kimataifa ameieleza nchi hiyo ya Afrika magharibi kuwa ni "kiwango cha dhahabu kwa demokrasia katika Afrika".
Rais huyo mpya aliliambia shirika la habari la AFP kwamba baada ya kubadilishana madaraka kwa njia ya amani nchini mwake na nchi kama Nigeria , viongozi wanaotaka kubakia madarakani kwa gharama yoyote "wanapambana na wimbi la historia".
Nchini Nigeria -- ikiwa inafahamika kwa ushindani katika uchaguzi na matokeo yake ya ghasia -- Goodluck Jonathan amefanya uamuzi mkubwa wa kumwachia madaraka Muhammadu Buhari mwaka 2015.
Lakini katika wiki aliyochaguliwa Akufo-Addo, rais aliyeshindwa Yahya Jammeh wa Gambia aliahidi kupinga matokeo ya uchaguzi ambapo hapo mwanzo alikubali kushindwa.
Kwingineko katika bara hilo, kuna mifano kadhaa ya viongozi wanaotaka kubadilisha katiba kuhakikisha wanabakia madarakani kwa miaka mingi zaidi.
Upatanishi Gambia
Buhari na viongozi wengine wa Afrika watakutana kwa mazungumzo baada ya sherehe za kuapishwa rais wa Ghana kujadili mzozo katika nchi ya Gambia unaosababishwa na kukataa kwa Jammeh kuondoka madarakani.
"Uamuzi muhimu kuhusiana na mkwamo huo unatarajiwa kuchukuliwa katika mkutano huo muhimu,"msemaji wa rais wa Nigeria Buhari , Garba Shehu aliwaambia waandishi habari mjini Abuja.
"Rais Buhari ni mpatanishi mkuu katika mzozo huo na anataka kuhakikisha kwamba mkwamo huo unatatuliwa.
Akufo-Addo ameapa kulirejesha taifa hilo la Afrika magharibi "katika njia yake ya maendeleo na ufanisi" baada ya kuporomoka kiuchumi chini ya Mahama hali iliyosababisha hatua za uokozi kutoka kwa shirika la fedha la kimataifa, IMF.
Wiki hii Mahama alitetea kazi yake, akisema serikali yake ilikumbana na , "upepo mkali" ambao ulisababisha ukuaji wa uchumi kupungua kasi, deni la serikali kupanda na sarafu ya cedi kuporomoka.
Lakini kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 58 amewahimiza Waghana kumpa ushirikiano Akufo-Addo na siku ya Jumatano alimtembeza na kumuonesha mrithi wake katika maeneo ya serikali, katika jengo la Flagstaff , mjini Accra.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Isaac Gamba