Cuba imeahidi kufanya uchunguzi kubaini sababu ya ajali
19 Mei 2018Cuba imeahidi kufanya uchunguzi kubaini sababu ya ajali ya ndege iliyouwa watu takribani 100 karibu na mji wake mkuu Havana hapo jana. Rais mpya wa nchi hiyo Miguel Diaz Canel aliitembelea sehemu ilikoanguka ndege hiyo, na kusema matukio yote yatafanyiwa uchunguzi na ripoti itatolewa.
Gazeti la serikali ya nchi hiyo la Granma limesema kuwa watu watatu walinusurika katika ajali hiyo, na kuongeza kuwa idadi kamili ya waliokufa ilikuwa 105. Aidha, gazeti hilo lilisema wahanga wengi walikuwa raia wa Cuba, lakini walikuwemo pia raia watano wa kigeni, pamoja na marubani kutoka nje ya nchi.
Ndege hiyo iliyopata ajali ilikuwa chapa Boeing 737 inayomilikiwa na Mexico. Jumla ya watu wanne, wanawake watatu na mwanamme mmoja walipatikana wakiwa hai baada ya ajali hiyo, lakini mwanamme huyo alifariki muda mfupi baadaye. Wanawake hao watatu bado wako katika hali mahtuti.