1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaepuka hatari ya kushindwa kulipa deni lake.

2 Juni 2023

Baraza la Seneti nchini Marekani limeuidhinisha mswada wa nchi hiyo kuhusu ukomo wa deni kwa kura 63 dhidi ya 36. Taifa hilo limeepuka hatari ya kushindwa kulipa deni lake la taifa.

https://p.dw.com/p/4S6Vy
US-Kapitol | Senat verhandelt Schuldenobergrenze
Picha: Senate Television/AP/dpa/picture alliance

Baraza la Seneti la Marekani limepitisha sheria ya pande mbili inayoungwa mkono na Rais Joe Biden ambayo imeiwezesha Marekani kuondoa ukomo wa kukopa kutokana na hapo awali nchi hiyo iliweza kukopa hadi dola trilioni 31.4 ambapo sasa itaweza kukopa zaidi. Hatua hiyo imeiepusha serikali ya rais Biden kushindwa kulipa deni la taifa.

Kiongozi wa Wengi katika Baraza la Seneti Chuck Schumer.
Kiongozi wa Wengi katika Baraza la Seneti Chuck Schumer. Picha: J. Scott Applewhite/AP Photo/picture alliance

Baraza la Seneti lilipiga kura 63 kwa 36 kuuidhinisha mswada huo ambao kwanza ulikuwa umepitishwa siku ya Jumatano tarehe 31 na Bunge la Wawakilishi, huku wabunge walipokimbizana na muda kufuatia miezi kadhaa ya mabishano ya vyama vya Democratic na Republican. Kiongozi wa Wengi katika Seneti Chuck Schumer amempongeza Rais Biden na timu yake kwa kufanikisha maelewano ya busara wakati ambapo Marekani ilikabiliwa na shinikizo kubwa.

Soma:Baraza la Wawakilishi Marekani lapitisha muswada wa ukomo wa kukopa

Ingawa maelewano yaliyofikiwa baada ya majadiliano kati ya rais Joe Biden na Spika wa Bunge Kevin McCarthy hayawaridhishi kabisa wanachama wa Republican au wenzao wa chama cha Democratic lakini matokeo, baada ya wiki kadhaa za mazungumzo ya bajeti yameliondoa suala la ukomo wa deni ambalo lilihatarisha kuuathiri uchumi wa Marekani na wa mataifa mengine duniani huku zikiwa zimesalia siku chache tu kabla ya taifa hilo kubwa kushindwa kulipa deni lake mnamo tarehe 5 Juni ambapo ingekuwa ni kwa mara ya kwanza Marekani kushindwa kutimiza majukumu yake ya kulipa deni.

Rais wa Marekani Joe Biden.
Rais wa Marekani Joe Biden.Picha: Saul Loeb/AFP

Mswada huo sasa unasubiri kutiwa saini na Rais Joe Biden. Biden amekaribisha kwa furaha kuidhinishwa mswada huo, amesema huo ni ushindi mkubwa kwa uchumi wa Marekani na watu wake na kwamba atautia saini haraka iwezekanavyo mara tu utakapotua mezani kwake. Masoko ya hisa duniani yameimarika leo kutokana na hatua ya pande mbili nchini Marekani kufikia makubaliano kuhusu ukomo wa deni nchini humo.

Vyanzo:AP/RTRE