Ahmadinejad ataka tena urais Iran
12 Aprili 2017Kwa kufanya hivi rais huyo wa kitambo ameupuza mwito wa uongozi wa kidini wa nchi hiyo kwamba asiwanie kiti hicho.
Ingawa hatua hiyo aliyochukua imeripotiwa na vyombo vya habari nchini humo kuwa kama hatua ya Ahmadinejad kuongeza umaarufu wa mwandani wake anayeiwania nafasi hiyo, ni hatua pia ya kumpa changamoto kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, aliyemuonya dhidi ya kuwasilisha ugombea wa urais.
Shirika la habari la Mehr lilimnukuu Ahmadinejad akisema amejiandikisha kama mgombea ili kumuunga mkono makamu wake wa kitambo Hamid Baghaie. Nalo shirika la habari la ILNA lilimnukuu akisema "Kiongozi Mkuu alinishauri nisiwanie urais. Kama mgombea nilikubali ushauri wake ingawa halikuwa sharti, bado nimejitolea kutimiza ahadi yangu."
Usajili kwa ajili ya uchaguzi huo wa Mei 19 ulianza Jumatatu na utadumu kwa kipindi cha siku tano ambapo baada ya hapo waliojisajili watakaguliwa kwa msingi wa kisiasa na kidini na baraza linalotoa mwongozo. Kufikia sasa watu 197 wamejisajili kwa uchaguzi huo, 8 miongoni mwao wakiwa wanawake ila hakuna mwanamke ambaye ashawahi kukubaliwa kusimama kuwania urais katika jamhuri hiyo ya Kiislamu.
Ahmadinejad alipoteza wafuasi wengi wa kihafidhina wakati wa utawala wake
Rais Hassan Rouhani mwenye msimamo wa kadri na aliyehusika katika kutia saini ule mkataba wa nyuklia wa Iran mwaka 2015 na mataifa yenye nguvu zaidi duniani, uliopelekea Iran kuondolewa vikwazo vya kimataifa vya kifedha na biashara, anatarajiwa kuwania nafasi ya kuchaguliwa tena ingawa anakabiliwa na ushindani mkali kutoka kwa wahafidhina wanaompinga.
Ahmadinejad alipoteza wafuasi wengi wa kihafidhina wakati wa utawala wake uliokuwa na utata, na wengine walisema Jumatano kwamba, kwa kwenda kinyume na amri ya Kiongozi wao Mkuu wa kidini ndio mwisho wake. Mbunge wa kitambo na mwaminifu wa Ahmadinejad, Mehdi Koochakzadeh aliandika katika mtandao wa kijamii, "kwa hatua ya leo ya kujiandikisha kama mgombea wa Urais, uaminifu wangu kwako umevunjika."
Mbunge wa zamani aliyekuwa katika kambi ya wahafidhina Elyas Naderan, ameandika kwenye mtandao wake wa kijamii wa Twitter, "mwisho wa Ahmadinejad."
Mchambuzi Farzan Sabet lakini anasema, huenda ikawa amefanya hivyo kusudi atoe kitisho katika hilo baraza la uongozi kwamba iwapo litamkataa Baghaei kama walivyoyafanya kwa mkuu wake wa zamani wa wafanyakazi wa umma Esfandiar Rahim Mashaei katika uchaguzi wa rais wa mwaka 2013, basi atagombea urais mwenyewe.
Rouhani ameuimarisha uchumi wa Iran ila kiwango cha ukosefu wa kazi kipale pale
Wahafidhina wamekuwa na wakati mgumu kumuunga mkono mgombea mmoja atakayeshindana na rais Hassan Rouhani anayetarajiwa kujisajili katika siku chache zijazo. Walifanya mkutano mkubwa wiki iliyopita ambapo walibuni orodha ya majina matano ambayo yatapunguzwa na jina moja pekee ndilo litakalosalia kabla uchaguzi huo, ingawa wengine miongoni mwao tayari wameshasema watawania kiti hicho kivyao bila chama.
Aliyekuwa juu katika orodha hiyo ni Ebrahim Raisi ambaye ni jaji na ambaye kwa sasa anaongoza ule wakfu wenye nguvu wa Reza katika mji mtakatifu wa Washia wa Mashhad.
Meya wa Tehran Mohamed Bagher Ghalibaf alikuwa kwenye orodha hiyo pia, ingawa haijabainika iwapo atasimama kwa mara ya tatu kuwania urais wa nchi hiyo.
Rouhani ameuimarisha uchumi wa nchi hiyo lakini Wairan wengi wameshushwa mabega na ukosefu wa uwekezaji katika uchumi na kiwango cha ukosefu wa kazi kinachosalia kuwa asilimia 12. Lakini uongozi wa Rouhani unadai ulirithi uchumi ulioharibika mno kutokana na sera mbaya za Ahmadinejad zilizojumuisha watu kupewa pesa kila mwezi pamoja na miradi mibovu ya nyumba.
Lakini sera hizi pia zimechangia kuhakikisha Ahmadinejad mwenye umri wa miaka 60 bado ana umaarufu hususan miongoni mwa maskini, jambo ambalo linahujumu jaribio la wahafidhina kuungana na kupata mgombea mmoja.
Iwapo Ahmadinejad atakubaliwa awanie urais, bila shaka atapata kura nyingi kutoka kwa wahafidhina kuliko Rouhani, alisema Farzan Sabet.
Mwandishi: Jacob Safari/AFPE/Reuters
Mhariri: Josephat Charo