Agizo la Museveni lazua mshangao Uganda
5 Desemba 2022Kwa mujibu wa agizo hilo la rais Yoweri Museveni linamaanisha kwamba mtu yeyote ambaye atahitaji huduma za serikali lazima awe amepata chanjo hiyo dhidi ya UVIKO-19.
Kulingana na asasi za kiraia, agizo hilo litaweza kutumiwa vibaya katika ukiukaji wa haki za binadamu pale mtu ambaye atahitaji huduma za serikali akikoseshwa fursa hiyo. Aidha hii inatoa mwanya kwa watu kupata vyeti bandia na kwa hiyo kutojali kupata chanjo.
Huku makali ya ugojwa huo yakiwa yamedhibitiwa vilivyo sehemu nyingi duniani kiasi kwamba si tishio tena kama ilivyokuwa, watu wengi nchini Uganda hawaoni kwa nini agizo hilo litiliwe mkazo. Wanapendekeza uhamasishaji uimarishwe ili watu wajue madhara ya kutopata chanjo lakini pia kuelimishwa kuwa ni salama kwa afya zao na za jamaa zao.
Kwa sasa angalau watu milioni 26 kati ya idadi jumla ya nchi hiyo ya watu milioni 45 wamepata chanjo hiyo. Ila serikali ingependa kufikia kiwango cha watu milioni 28, idadi ambayo inadhani itakuwa nzuri kuepusha kurejea kwa mripuko wa ugonjwa hatari wa UVIKO-19.