Afrika yazidi kukua, lakini umaskini bado
30 Mei 2014Si jambo la bahati mbaya kuwa mkutano wa Africa Rising, au Afrika inainukia umefanyika nchini Msumbiji. Ikiwa na ukuaji wa uchumi wa zaidi ya asilimia 7 kwa mwaka, msumbiji ni moja ya mataifa yanayokuwa kwa kasi kubwa zaidi duniani, na inawakilisha nguvu mpya ya bara la Afrika.
Makampuni mengi yanavutiwa kuwekeza nchini Msumbiji kutoka na hifadhi kubwa ilizonazo na gesi asili na makaa ya mawe. Nchi hiyo imetoka kuwa taifa lisilovutia na maskini kusini mwa Afrika, na kuwa la tatu kwa kuvutia uwekezaji wa nje kusini mwa jangwa la sahara.
Manufaa kwa wachache
Mkurugenzi mkuu wa shirika la IMF Christine Lagarde, anasema uvumbuzi wa hivi karibuni wa maliasili ni fursa kubwa sana kwa Msumbiji, na nunaweza kutumiwa kwa namna inayoleta manufaa kwa taifa zima, lakini anaonya pia kwamba uvumbuzi huo unaweza kutumiwa vibaya.
"Mara nyingi mapato yatokanayo na maliasili hizi hayatumiki kwa manufaa ya waliyowengi. Kwa bahati mbaya yanahodhiwa na watu wachache na kutowafikia raia wote," anasema Lagarge.
"Uchimbaji unaweza kuchangia kiwango kikubwa katika mauzo ya nje, lakini huchangia kidogo kwenye mapatao ya bajeti na uzalishaji wa ajira na baadaye ufadhili wa mapengo ya kimiundombinu."
Miundombinu, miundombinu
Ujenzi wa minudombinu ndiyo mada kuu ya mkutano wa Africa Rising unaofanyika jana na leo katika mji mkuu wa Msumbiji Maputo. Makamu wa rais wa Mfuko wa China kwa ajili ya maendeleo ya Afrika Wang Yong alisema anaamini miundombinu ndiyo msingi wa maendeleo ya sekta nyingine zote.
Lakini Bibi Clair Short, waziri wa zamani wa maendeleo wa Uingereza, na mwennyekiti wa sasa wa shirika la kusimamia uwazi katika sekta ya madini - Extractive Industry Transparency Initiative EITI, alikosoa mtizamo wa kutilia tu mkazo sekta ya miundombinu, na kutoa wito kwa serikali kuzingatia pia uboreshaji wa hali za raia maskini.
Kwa miaka kadhaa EITI imekuwa ikiendesha kampeni ya kuhakikisha uwazi katika sekta ya rasilimali zinazochimbwa ardhini, na mataifa mengi ikiwemo Msumbiji, yamejiunga na mfumo wake na sasa yanachapisha takwimu ambazo huko nyuma zilikuwa ni siri.
Uwazi na ajira
Hata kamati ya maendeleo ya Afrika, iliyoanzishwa na katibu mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan, inaamini kuwa mapato yatokanayo na rasilimali za ardhini yataweza kunuwanufaisha waafrika wengi ikiwa kutakuwepo na uwazi zaidi katika sekta hiyo.
Serikali za Msumbiji na Uganda zimesema kuwa zinahakikisha uwazi zaidi katika kujadili mikataba na makumpuni yanayotaka kuwekeza katika sekta za uchimbaji, ili kuhakikisha kuwa si tu serikali zinapata mapatao yanayostahiki, lakini pia kuhakisha kuwa kunakuwepo na ajira za kutosha kwa wananchi.
Mwandishi: Johannes Beck
Tafsiri: Iddi Ssessanga
Mhariri: Josephat Charo.