Afrika Kusini yasema askari wake wawili wameuawa DR Kongo
15 Februari 2024Afrika Kusini imesema leo kuwa askari wake wawili wameuawa na kombora mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Hivyo ndio vifo vya kwanza kutokea tangu nchi hiyo ilipopeleka wanajeshi wake Kongo kusaidia kupambana na uasi.
Jeshi la Afrika Kusini limesema wanajeshi wengine watatu walijeruhiwa katika tukio hilo la jana karibu na mji wa mashariki wa Goma. Limesema kombora lilianguka ndani ya vituo vya kijeshi vya Afrika Kusini. Nchi hiyo ilipeleka askari 2,900 mashariki mwa Kongo katikati ya Desemba mwaka jana.
Soma pia: Kongo na SADC kuanzisha operesheni ya pamoja
Walitumwa kama sehemu ya jeshi la kikanda la Kusini mwa Afrika, linalojumuisha pia askari kutoka Malawi na Tanzania, lililopewa jukumu la kuisaidia serikali ya Kongo kupambana na waasi wa M23.
Makabiliano yameongezeka katika siku za karibuni karibu na mji wa kimkakati wa Sake, ambao unapatikana karibu kilomita 20 kutoka Goma.