Afrika Kusini yakana Mandela hana fahamu
5 Julai 2013Kifungu kinachoelezea hali mbaya ya Mandela kilitumika katika nyaraka za mahakama zilizowasilishwa na jamaa wa familia ya Mandela, kwa mujibu wa wakili aliyenukuliwa na vyombo vya habari. Ofisi ya rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, ilisema madaktari wanakana rais huyo wa zamani amepoteza kabisa fahamu na hali hiyo haitabadilika. Zuma alisema jana mchana baada ya kumtembelea hospitalini kuwa Madiba anapewa matibabu ya hali ya juu na timu ya madaktari bingwa waliobobea katika taaluma ya utabibu, ambao wako kando ya kitanda chake hospitalini kila wakati.
Nyaraka za mahakama zilizopatikana na shirika la habari la AFP zinaonyesha madaktari wanaomtibu Mandela walisema hana fahamu na kuishauri familia wiki moja iliyopita iruhusu mashine zinazomsaidia kuishi zizimwe ili apumzike. Badala ya kuyarefusha mateso dhidi yake familia ya Mandela inatafakari juu ya pendekezo hili kama jambo linalowezekana, ilisema taarifa hiyo. Kwa mujibu wa wakili wa familia, Wesley Hayes, waraka huo ulikuwa sehemu ya jitihada za kuifanya mahakama isikilize kesi kuhusu mahala pa mwisho yatakakozikwa mabaki ya watoto watatu wa Mandela.
Tangu nyaraka hizo kuwasilishwa mahakamani serikali ya Afrika kusini, jamaa wa familia na marafiki wa karibu wamekuwa wakiripoti juu ya hali ya Mandela kuendelea kuwa nzuri, japo kidogo. Katika taarifa yake ya kwanza kwa umma hapo jana, mke wa Mandela, Graca Machel, alisema na hapa tunanukuu; "Ingawa Madiba wakati mwingine anaonekana kusumbuka, mara chache anakuwa na maumivu, lakini hajambo," mwisho wa kunukuu. Graca pia alitoa mwito kuwe na umoja nchini.
Tutu asihi jina la Mandela lisichafuliwe
Wakati huo huo, mshindi wa zamani wa tuzo ya amani ya Nobel, askofu mstaafu Desmond Tutu, ameisihi familia ya Mandela isilichafua jina la shujaa huyo kufuatia mzozo kuhusu mahala walikozikwa watoto wa Mandela. "Tafadhali, tafadhali, tafadhali, tusifikirie tu kuhusu sisi wenyewe. Ni kama kumtemea mate Mandela usoni," alisema Tutu katika taarifa aliyoitoa. "Tunataka tuwakumbatie, tuwasaidie, tuonyeshe upendo wetu kwa Madiba kuptia ninyi," aliongeza Desmond Tutu.
Familia ya Mandela imekabiliwa na mgogoro mkali wa kisheria kuhusu kuzikwa tena mabaki ya watoto wa kiongozi huyo wa zamani, ambayo yalifukuliwa kutoka makaburi ya familia huko Qunu mnamo mwaka 2011 na kuzikwa katika kijiji cha Mvezo. Mabaki hayo yalifukuliwa na mjuu mkubwa wa Mandela, Mandla, bila ridhaa ya familia. Mabaki hayo yalizikwa upya jana katika kijiji cha Qunu, alikokulia Mandela baada ya jamaa wa familia yake, wakiongozwa na mtoto wa kike wa Mandela, Makaziwe, kwenda mahakamani kuitaka imlazimishe Mandla ayarudishe mabaki hayo.
Mwandishi: Josephat Charo/AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman