ANC kuunda serikali ya umoja na vyama vidogo vya kisiasa
5 Juni 2024Chama tawala cha Afrika Kusini, ANC, kinategemea kuunda serikali ya umoja wa kitaifa na vyama mbalimbali vya kisiasa nchini humo, baada ya kushindwa kupata wingi wa kutosha kuweza kutawala peke yake baada ya uchaguzi wa Mei 29, ambapo wapigakura wamekinyang'anya udhibiti wa bunge.
Soma pia:Ramaphosa apigia debe umoja baada ya matokeo mabaya ya ANC
Msemaji wa ANC, Mahlengi Bhengu-Motsiri amewaambia waandishi wa habari kuwa chama hicho kimekuwa kikizungumza na vyama vitano vya siasa, kuanzia chama cha kiliberali cha Democratic Alliance (DA) hadi chama cha siasa kali za mrengo wa kushoto, EFF.
Mikakati inayoweka ANC baada ya matokeo mabaya
Amesisitiza kwamba Rais Cyril Ramaphosa, ambaye ni kiongozi wa chama cha ANC atasalia kwenye wadhifa huo. Amesema Ramaphosa ameongoza chama cha ANC na Afrika Kusini vizuri sana na kwamba hawatamhusisha mtu yeyote aliye na mawazo kuingia katika muungano nao kwa masharti kwamba wamuondoe Rais Cyril Ramaphosa.
Ikilinganishwa na matokeo ya chaguzi zilizopita, matokeo ya wiki iliyopita yanaonyesha kupungua kwa uungwaji mkono kwa ANC. Fikile Mbalula, katibu mkuu wa chama cha (ANC), amesema pamoja na kuwa kuna mambo kadhaa yamechangia kupungua kwa uungwaji mkono, matokeo hayo yanatuma ujumbe wa wazi kwa ANC, na wangependa kuwahakikishia wananchi wa Afrika Kusini kwamba wamewasikia.
Soma pia: Nani atashirikiana na ANC kuunda serikali Afrika Kusini?
"Katika siku chache zijazo, ANC itakuwa na majadiliano katika chama na pamoja na vyama vingine na wadau kuhusu namna bora ya kuanzisha serikali za kitaifa na za majimbo zinazoakisi matakwa ya wananchi, na zinazoweza kuipeleka nchi mbele," ameeleza Fikile.
ANC imesema kwamba imejaribu kukifikia chama kipya cha uMkhonto we Sizwe (MK) cha Rais wa zamani Jacob Zuma kwa mazungumzo, lakini "hakijapata majibu chanya."
Kauli ya vyama vinavyolengwa kwa mazungumzo
Zuma ni kiongozi wa zamani wa ANC ambaye alikihama chama hicho na kumkosoa vikali Rais wa sasa Cyril Ramaphosa. Ingawa ANC inafanya majadiliano na vyama vingine katika jaribio la kuunda serikali ya "umoja wa kitaifa" na muungano rasmi, inasema hilo sio chaguo pekee.
Chama cha Zuma, ambacho kimepata asilimia 14.6 ya kura zote, kimekataa matokeo ya uchaguzi na kutishia kususia bunge. Pia imesema haitaunga mkono serikali inayoongozwa na ANC ikiwa Ramaphosa ataendelea kushikilia usukani.
Soma pia: Chama cha ANC kuanza kuunda serikali ya mseto
Tayari chama cha kiliberali cha DA kimesema hakitajiunga na serikali ambayo itawashirikisha pia Umkotho Wesizwe na EFF.
Chama cha ANC kimeiongoza Afrika Kusini tangu Rais wa kwanza mweusi wa Afrika Kusini Nelson Mandela kukiingiza madaraka katika uchaguzi wa 1994 ulioashiria mwisho wa ubaguzi wa rangi, lakini wapiga kura waliadhibu wakati huu kwa umaskini unaoendelea na ukosefu wa ajira, uhalifu uliokithiri, rushwa na ukataji wa umeme mara kwa mara.