1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magazeti ya Ujerumani

16 Februari 2018

Hatimae Jacob Zuma ameng'atuka baada ya kushinikizwa na chama chake cha ANC.na hapo Alhamisi rais mpya Cyril Ramaphosa aliapishwa rasmi kuwa rais wa Afrika Kusini ni baadhi ya yalioandikwa magazetini.

https://p.dw.com/p/2soU3
Südafrika - neuer Präsident Cyril Ramaphosa - Vereidigung
Picha: Reuters/M. Hutchings

Die zeit

Gazeti la Die Zeit linasema Ramaphosa ni mwanasiasa mwenye sifa nyingi. Ramaphosa pia anao mahasimu, lakini wote wanatambua umahiri wake katika kufanya mazungumzo kwa ustadi. Ramaphosa anao uwezo mkubwa wa kuwasoma mahasimu wake na inapobidi anapiga hatua mbili nyuma. Gazeti hilo linatilia maanani kwamba Ramaphosa ni mwanasiasa tajiri linasema pia mwanasiasa huyo anaweza kuwa mkarimu lakini pia anaweza kuwa mkali.

die tageszeitung

Gazeti la die tageszeitung limeandika juu ya msako uliofanywa na polisi kwenye nyumba ya familia ya akina Gupta mjini Johannesburg. Kaka mkubwa wa familia hiyo, Ajay Gupta alikamatwa.Gazeti hilo linasema msako huo ulifanyika wakati watu nchini Afrika Kusini walipokuwa wanasubiri jibu la Jacob Zuma kuhusu chama chake kumtaka ajiuzulu. Die tageszeitung linatilia maanani kuwa msako huo ulikuwa ishara thabiti ya kumtangazia vita bwana Zuma dhidi ya mfumo wake wa kifisadi.

Die tageszeitung linaeleza kwamba tangu Zuma alipoingia madarakani mnamo mwaka 2009, familia ya akina Gupta, ya ndugu watatu, wafanya biashara wakubwa, imekuwa na usemi mkubwa sana katika mambo ya serikali ya Afrika kusini, kiasi cha kuwafanya watu nchini humo waseme kuwa serikali yao imetekwa. Kandarasi thamani ya mabilioni ya fedha, zilizotolewa na serikali, zimeenda kwa kampuni za familia hiyo kwa kushirikiana na jamaa wa Zuma ikiwa pamoja na mwanawe Duduzane Zuma mwenye umri wa miaka 35.

Gazeti la hilo linafahamisha kwamba mtoto huyo wa Zuma aliingia mafichoni polisi walipofanya msako kwa akina Gupta. Polisi walifanya msako huo ili kuchunguza madai juu ya kutoweka kiasi kikubwa cha fedha, zilizotolewa na serikali ya jimbo kwa ajili ya kuwapatia wakulima wadogo wadogo. Kwa mujibu wa taarifa iliyokaririwa na gazeti la die tageszeitung, fedha hizo ziliingia katika mikono ya kampuni inayoitwa Estina yenye uhusiano na akina Gupta. Fedha hizo dola milioni 10 hatimaye ziliingia katika akaunti ya akina Gupta katika benki moja ya Dubai.

Neues Deutschland

Nalo gazeti la Neues Deutschland wiki hii limeandika juu ya kukwama kwa mchakato wa amani nchini Mali. Gazeti hilo linasema licha ya msaada wa kijeshi unaotolewa na jumuiya ya kimataifa hakuna uhakika wa usalama nchini Mali. Gazeti hilo  linatufahamisha. Mkataba wa amani ulitiwa saini mnamo mwaka  2015 nchini Mali. Kulingana na mkataba huo serikali ya nchi hiyo ilipaswa kurejeshewa udhibiti wa nchi yote baada ya sehemu ya kaskazini ya nchi hiyo kutekwa na kukaliwa na mfungamano wa wapiganaji wa Kituareg na wanaitikadi kali wa Kiislamu. Mnamo mwaka 2013 majeshi ya Ufaransa yaliingilia  kati na kuwatimua waasi hao.  

Gazeti hilo la Neues Deutschland linasema licha ya hatua hiyo iliyochukuliwa na majeshi ya Ufaransa, idadi ya makundi   yenye silaha imeongezeka nchini Mali. Licha ya kuwepo wanajeshi  wa Ufaransa 1000 na walinda amani wa Umoja wa Mataifa 13,000 hakuna wiki inayopita, nchini Mali bila ya kufanyika shambulio.

Gazeti hilo la Neues  Deutschland limemnukuu aliyekuwa mshauri wa rais juu ya mchakato wa amani, Nafet Keita akieleza kuwa hali imezidi kuwa mbaya katika kipindi  cha miaka mitano iliyopita nchini humo. Mali haina uwezo wa kutawala kwa uhakika katika sehemu ya Kaskazini. Madhali serikali haiwezi kutekeleza sera yake bila ya ushawishi kutoka nje haitakuwa rahisi kuleta amani nchini Mali.

Jeshi la Mali haliwezi kufika katika sehemu fulani za nchi kwa sababu kwanza ni lazima lipate ridhaa ya kundi la Barkhane (yaani mfungamano wa majeshi ya kulinda amani nchini Mali) yanayoongozwa na Ufaransa. Mshauri huyo wa rais wa zamani bwana Keita amesema amani haitapatikana kwa njia ya upanga tu. Amesema ni lazima mdahalo ufanyike wa kuzishirikisha pande zote.

Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen

Mhariri:Yusuf Saumu