Afrika katika magazeti ya Ujerumani
17 Novemba 2017Gazeti la Die Landeszeitung linatuhumu kwamba Rais Robert Mugabe ameangushwa na mkono unaotokea mbali. Linasema Jenerali aliyeziongoza hatua za kumwangusha Mugabe alialikwa China siku chache tu kabla ya hapo. Gazeti hilo linasema, ni muda mrefu sasa tangu sarafu ya China (Yuan) ianze kutumika rasmi nchini Zimbabwe. Gazeti hilo linasema jeshi linakataa kuiita hatua yake kuwa ni mapinduzi ili kuepusha vikwazo kutoka jumuiya ya maendeleo ya nchi za kusini mwa Afrika SADC.
Nalo gazeti la Reutlinger General-Anzeiger linakubaliana na tuhuma hizo na linaeleza kwamba China inawekeza mabilioni nchini Zimbabwe kwa sababu inayataka madini ya nchi hiyo. Na kwa hivyo mtu anaweza kutuhumu kwamba atakayechukua nafasi ya Mugabe atakuwa mtu atakaye wakosha roho Wachina.
Badischen Neuesten Nachrichten
Gazeti hilo halina matumaini makubwa juu ya majenerali wa Zimbabwe. Linasema lengo la majenerali hao ni kuyalinda maslahi yao, baada ya Mugabe kuondolewa. Wanajeshi hao hawajali hata chembe kwamba Mugabe aliigeuza Zimbabwe kuwa nyumba ya masikini Kusini mwa Afrika. Ni jambo la kulitilia mashaka iwapo kundoka kwa Mugabe kutawaletea neema watu wa Zimbabwe.
Die tageszeitung
Mwandishi wa gazeti hilo Dominic Johnson anasema dunia imeshuhudia wasaa wa kihistoria. Baada ya kutawala kwa miaka zaidi ya miaka 37 enzi ya Mugabe imefikia mwisho. Hata hivyo katika kipindi hicho Mugabe alikuwa na usemi, siyo tu nchini mwake bali barani Afrika kote.
Mwandishi wa die tageszeitung anasema uzito wa kisiasa wa Mugabe barani Afrika haukuwa wa kawaida. Kwanza alishinda vita vya ukombozi na baadae alisimama mstari wa mbele katika kuzikabili siasa za nchi za Magharibi. Mwandishi Dominc Johnson anasema Mugabe alizipa kisogo nchi za Magharibi ili kuonyesha muamko mpya wa kisiasa wa Waafrika. Licha ya kuiangusha nchi yake kiuchumi katika namna ya kushtusha jina la Mugabe litaingia katika vitabu vya historia na kukumbukwa kama mzalendo adhimu wa bara la Afrika.
Mabadiliko yaa hali ya hewa
Hali ya hewa barani Afrika inawaweka watu wa bara hilo kati ya mvua kubwa na ukame. Gazeti la Der Tagesspiegel limemnukuu Constance Okollet kutoka Uganda, akielezea juu ya hali hiyo kwenye mkutano wa mjini Bonn ambapo wajumbe kutoka duniani kote waliyajadili masuala ya mabadiliko ya hali ya hewa. Gazeti hilo limemnukuu mama huyo ambaye ni mkulima , akisema, wakulima wa Afrika hawakusababisha mabadiliko ya tabia nchi lakini wao ndio wanaoadhibiwa. Akikumbuka yaliyotukia kwenye kijiji chake mnamo mwaka wa 2007, Okollet aliwaambia wajumbe kwenye mkutano huo kwamba alifikiri Mungu aliwaadhibu wanakijiji hao. Bi Okollet alielezea kuwa baada ya kunyesha mvua kubwa ulifuatia ukame uliounguza mazao yao yote. Wajumbe kutoka Afrika waliohudhuria mkutano wa mazingira mjini Bonn walipigia debe uwezekano wa kupatiwa msaada mkubwa zaidi wa fedha ili kujiweka sawa na hivyo kuweza kuzikabili athari za mabadiliko ya hali ya hewa. Hata hivyo gazeti hilo la Der Tagesspiegel linatilia maanani mfuko wa fedha uliopo sasa kwa ajili ya kuwasaidia wakulima wa Afrika ambao ulianzishwa kwa mujibu wa rasimu ya Kyoto inayofikia mwisho wake mwaka wa 2020. Gazeti linasema mustakabali wa mfuko huo umo mashakani.
die tageszeitung
Makala nyingine ya gazeti la die tageszeitung inazunngumzia hatua ya ujasiri iliyochukuliwa na rais mpya wa Angola Joao Lourenco ya kumwondoa kwenye madaraka tajiri mkubwa sana barani Afrika, Isabel dos Santos binti wa rais wa zama wa nchi hiyo Eduardo dos Santos. Gazeti hilo la die tageszeitung linafahamisha kuwa rais Joao Lourenco amemwondoa Isabel Santos kwenye uongozi wa kampuni ya mafuta - Sonangol inayomilikiwa na serikali ya Angola. Isabel anayekadiriwa kuwa na utajiri wenye thamani ya zaidi ya dola Bilioni tatu, aliteuliwa mnamo mwaka 2016 kuwa mkuu wa kampuni hiyo ya mafuta. Isabel aliteuliwa na baba yake, Dos Santos aliyekuwa rais wa Angola kuanzia mwaka 1979 hadi kuondolewa kwake mwaka huu wa 2017.
Gazeti hilo linatilia maanani kwamba rais mpya wa Angola Joao Lourenco amechukua hatua za kutia moyo tangu alipoingia madarakani. Amewaengua vigogo wengi waliokuwa mashuhuri katika medani ya siasa nchini humo.
Mwandishi: Zainab Aziz/Deutsche Zeitungen
Mhariri: Saumu Yusuf