Afisa wa ngazi ya juu wa China ziarani Korea Kaskazini
12 Aprili 2024Matangazo
Taarifa za safari hiyo ya Zhao Leji, ambaye ni mwenyekiti wa Bunge la China na anayezingatiwa kuwa kiongozi wa tatu kwa nguvu ya madaraka ndani ya chama tawala cha kikomunisti, zimetolewa na shirika la habari la Korea Kaskazini.
Tayari amekutana na mwenzake Choe Ryong Hae na kujadili njia ya kutanua mahusiano na kubadilishana uzoefu kwenye uga wa siasa, uchumi na utamaduni.
Inaarifiwa mashauriano hayo ndiyo ya ngazi ya juu zaidi kati ya viongozi wa pande hizo mbili ndani ya kipindi cha miaka mitano iliyopita. Yamefanyika katika wakati serikali mjini Pyongyang inajaribu kuboresha usuhuba wake na China pamoja na Urusi chini ya kiwingu cha kutengwa kimataifa na mbinyo kutoka Marekani na washirika wake wa magharibi.