Ghani na Abdullah wasaini makubaliano ya kugawana madaraka
17 Mei 2020Rais wa Afghanistan Ashraf Ghani na hasimu wake Abdullah Abdullah Jumapili wamesaini makubaliano ya kugawana madaraka, na kumaliza mzozo ulioendelea kwa miezi kadhaa hadi kulitumbukiza taifa hilo katika mgogoro wa kisiasa.
Soma zaidi: Ghani na hasimu wake Abdullah wakaribia kupatana
Msemaji wa Ghani Sediq Sediqqi, ameandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba Abdullah ataongoza Tume ya Kitaifa ya Maridhiano na wanachama wa timu yake watajumuishwa kwenye baraza la mawaziri.
Hatua hiyo imefanikishwa wakati ambapo Afghanistan inapambana na msururu wa migogoro iliyolikumba taifa hilo, ikiwa ni pamoja na kuenea kwa haraka kwa maambukizi ya virusi vya corona pamoja na ongezeko la vurugu zinazofanywa na wanamgambo ambapo watu kadhaa waliuawa katika shambulio la kikatili wiki iliyopita.
Chini ya mpango wa awali wa kugawana madaraka, Abdullah Abdullah aliwahi kuwa na wadhifa wa 'mtendaji mkuu', lakini aliupoteza wadhifa huo baada ya kushindwa katika uchaguzi wa rais uliompa ushindi Ghani mnamo mwezi Septemba- mchumi wa zamani wa Benki ya Dunia - licha ya madai ya upinzani kwamba uchaguzi huo ulikuwa na udanganyifu.
Abdullah, alijitangaza kuwa rais na kuapishwa mnamo Machi 9, siku ambayo Ghani pia aliapishwa tena kama rais.
Abdullah kuongoza mazungumzo na Taliban
Siku ya Jumapili wapinzani hao wawili walikubaliana juu ya mpango mpya wa kugawana madaraka, ambao wataalam wanahisi unaweza kuisaidia Afghanistan kujikomboa kutoka katika mzozo wa kisiasa.
Makubaliano hayo yanamtaja Abdullah kuongoza mazungumzo ya amani na kundi la Taliban katika siku za usoni, ambao tayari wamesaini makubaliano ya kihistoria na Marekani ili kusafisha njia ya kuondolewa kwa vikosi vya kigeni kutoka Afghanistan.
Soma zaidi: Wanajeshi wa Marekani waanza kuondoka nchini Afghanistan
"Hivi sasa inatarajiwa viongozi hawa watasuluhisha matatizo ambayo Afghanistan inakabiliana nayo, kama vile maambukizi ya virusi vya corona na mazungumzo ya amani na Taliban," Mchambuzi wa siasa kutoka Kabul Sayed Nasir Musawi ameliambia shirika la habari la AFP. Ameongeza kwamba ni shinikizo kubwa la Marekani ambalo limewalazimisha wanasiasa hao wawili kuamua kuafikiana juu ya mpango huo mpya wa kugawana madarakani.
"Lakini ni hatua ngumu...tofauti zitabaki kuwepo hadi pale watakapofikia makubaliano na kundi la Taliban."
Mnamo mwaka 2014, Abdullah na Ghani pia waligombea urais na baadae wote wawili wakadai ushindi. Ili kuepusha kuzuka mgogoro nchini humo, waziri wa wakati huo wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry aliingilia kati na kuwapatanisha wanasiasa hao wawili, hadi wakafikia makubaliano na Abdullah akapewa wadhifa wa mtendaji mkuu wa nchi.
Shinikizo la Marekani lafanikisha makubaliano
Lakini kufuatia mzozo sawa na huo uliotokea tena mwezi Machi baada ya uchaguzi mwengine, waziri wa sasa wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo hakuwa na subira na aliwakasirikia viongozi hao wawili kwa kushindwa kufikia makubaliano, na akatangaza kusitisha msaada wa dola bilioni 1 kwa Afghanistan.
Hatua hiyo ilikuwa pigo kubwa kwa Afghanistan, taifa maskini lenye pato la Taifa la dola bilioni 20 tu, na uchumi unaotegemea wafadhili.
Hatua hizo kali za Marekani zinatokana na msimamo wa rais wake Donald Trump ambaye ameahidi kwamba kipaumbele cha serikali yake ni kumaliza vita hivyo vya muda mrefu vya Marekani nchini Afghanistan.
Soma zaidi: Marekani yaitaka Taliban kusitisha mapigano
Mnamo mwezi Februari, Marekani ilisaini makubaliano na Taliban ambayo yaliahidi Marekani na washirika wake wa kigeni wataondoa vikosi vyote kutoka Afghanistan ifikapo mapema 2021. Kwa upande wake, kundi la Taliban lilikubali kutowashambulia wanajeshi wa kigeni.
Lakini mapigano kati ya vikosi vya Taliban na Afghanistan yanaendelea kuitikisa mikoa tofauti nchini humo, huku pande zote mbili zikitishia kuendelea kufanya ghasia baada ya mashambulio mawili wiki iliyopita ambayo yalisababisha vifo vya watu kadhaa, ikiwa ni pamoja na akina mama na watoto wachanga wakati watu waliokuwa na silaha walipovamia hospitali huko mjini Kabul. Kundi la Taliban limekana kuhusika na shambulio hilo la hospitali, ambalo Marekani imesema waliohusika ni kundi linalojiita Dola la Kiislam IS.
Vyanzo: (afp,dpa)